Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Awasili Mkoani Mtwara kwa Ziara ya Kikazi
Jul 24, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango, leo Julai 23, 2021 amewasili mkoani Mtwara kwaajili ya ziara ya kikazi ya siku tano.


Akiwa wilayani Masasi Makamu wa Rais amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Jenerali Marco Gaguti pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brig. Jenerali Wilbert Ibuge. Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geofrey Mwambe, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara pamoja na viongozi wa ulinzi na usalama.

Akitoa taarifa fupi kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Jenerali Marco Gaguti amesema mkoa huo unaendelea kuimarisha ulinzi na usalama hasa maeneo ya mipakani ili wananchi wafanye shughuli za kiuchumi kwa usalama na Amani. Akitoa taarifa ya mwenendo wa zao la korosho, Mkuu wa Mkoa amesema mkoa wa Mtwara unatarajia kuvuna korosho tani laki mbili na elfu themanini katika msimu ujao.

Makamu wa Rais amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuendelea kuchukua hatua kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19 na kuwahimiza msisitizo huo uendelee katika ngazi zote za uongozi katika mkoa huo.


Aidha, Makamu wa Rais amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia ukusanyaji mapato na kuzingatia matumizi ya mapato hayo ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Hapo kesho Julai 24, 2021 Makamu wa Rais anatarajiwa kushiriki misa ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha hayati Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa katika Kijiji cha Lupaso Wilaya ya Masasi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi