Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kuhakikisha miradi yote ya maboresho ya bandari ya Tanga inakamilika ifikapo mwezi Aprili, 2023 ili bandari hiyo ianze kufanya kazi kwa ufanisi na kuruhusu meli kubwa zaidi kuanza kutumia bandari hiyo.
Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gati mbili pamoja na uongezaji kina kutoka mita 3 hadi 13 unaondelea katika Bandari ya Tanga. Amesisitiza ni lazima bandari hiyo iweze kufanya kazi kwa viwango na kuvutia zaidi watumiaji wa bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Pia amemuagiza Meneja wa Bandari ya Tanga kushughulikia haraka malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu utendaji wa bandari hiyo ikiwemo kuchukua muda mrefu wa utokaji wa mizigo inayopita katika bandari hiyo ikilinganishwa na bandari nyingine za jirani. Amesema mapungufu hayo katika bandari ya Tanga yamepelekea wafanyabishara kutumia bandari za nchi Jirani na hivyo kulikosesha taifa mapato ambayo yangetumika kuwahudumia wananchi.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha uchunguzi unaoendelea wa kuungua moto kwa ghala la mali za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) la forodha. Amesema unahitajika uchunguzi wa kina ili kubaini wote waliohusika katika kusababisha hasara iliojitokeza katika ghala hilo. Pia amewataka viongozi wa TRA kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza mapato pasipo kuwanyanyasa wafanyabishara.
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi mbalimbali mkoani Tanga kuwa na ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza na kuhakikisha wanakomesha biashara ya dawa za kulevya, magendo,uvuvi haramu, uhamiaji haramu pamoja na biashara haramu ya binadamu.
Aidha amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga kusimamia wale wote wanaopaswa kujibu hoja zilizoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha wanajibu hoja hizo haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na ubadhirifu wa fedha za umma.
Miradi ya Maboresho ya Bandari ya Tanga inagharimu Shilingi bilioni 429 na inatarajiwa kuongeza ufanisi kufikia kuhudumia tani milioni 3 kwa mwaka kutoka tani laki saba na hamsini za sasa.