Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari MAELEZO

Makamu wa Rais Aongoza Kikao cha Pamoja SMZ na SJMT

Dec 06, 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amepongeza timu ya watalaamu pamoja na wajumbe wa kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zilizofanyika kupunguza kero nne kati ya Nane za Muungano zilizokuwa zimebaki tangu kufanyika kwa kikao hicho Agosti mwaka 2021.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifunga kikao cha kamati ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa wa Kambarage, Treasury Square Jijini Dodoma leo tarehe 06 Desemba, 2022. Amesema Kamati hiyo ni chombo muhimu katika kukuza undugu, ushirikiano,⅞ biashara na uchumi pamoja na kukuza umoja na tamaduni za wananchi wa pande zote mbili za muungano.

Makamu wa Rais amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kujadili hoja zilizobaki kwa nia za kujenga na kuimarisha muungano kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Aidha Makamu wa Rais amewasihi wajumbe wa kamati ya pamoja kuendelea na jitihada za kuongeza maarifa juu ya Muungano ikiwemo kusoma vitabu ili kuweza kuulinda na kuutetea vema muungano.

Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kikao hicho ni pamoja na malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapoagiza mizigo kutoka nje ya nchi na kupeleka Tanzania bara, hoja ya kodi ya mapato na kodi ya zuio, hoja ya ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO pamoja na hoja ya mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal III).

Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Said , Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka pande zote za Muungano, Makatibu na Manaibu Makatibu wakuu, Wakuu wa taasisi mbalimbali pamoja na Sekretarieti ya Kamati ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi