Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Ajiandikisha Daftari la Wapiga Kura Buhigwe
Oct 11, 2024
Makamu wa Rais Ajiandikisha Daftari la Wapiga Kura Buhigwe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akijiandikisha wakati wa ufunguzi wa zoezi la Uandikishaji kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kitongoji cha Kihanga Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 12 Oktoba, 2024.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameshiriki zoezi la uandikishaji kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kitongoji cha Kihanga Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma leo tarehe 12 Oktoba 2024.

 

Akizungumza na wanakijiji wa Kasumo mara baada ya kujiandikisha, Makamu wa Rais amesema zoezi la kujiandikisha katika daftari la kupiga kura ni muhimu kwa kuwa ni wajibu kushiriki katika kuchagua viongozi watakaoweza kuwasaidia wananchi. Amesema viongozi wa serikali za mitaa ndiyo wanaoishi jirani zaidi na wananchi hivyo ni muhimu kushiriki katika kuwachagua wale watakaolinda maslahi ya jamii husika.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba upatikanaji wa viongozi wazuri unaanza kwa kujiandikisha na baadaye kujitokeza kupiga kura hivyo amewasihi kushiriki kikamilifu katika mazoezi yote ya uchaguzi yanayotarajiwa hivi karibuni.

 

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito wa kipekee kwa wanawake kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa wanazifahamu vema changamoto za jamii na pia wanao uwezo wa kuongoza vizuri.

Amesisitiza wananchi kushiriki vema chaguzi zote kwa amani na utulivu kwa kujiepusha na lugha zisizo na staha pamoja na vurugu wakati wa kampeni. 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi