Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Ahutubia Mkutano wa UN Sweden
Jun 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 2 Juni, 2022 ameshiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unaoendelea nchini Sweden. 

Katika mkutano huo, viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wawakilishi wa jumui ya za kimataifa, wametoa ahadi pamoja na mapendekezo mbalimbali ya namna ya kukabilianana uharibifu wa mazingira duniani.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Dkt. Mpango amesema ili kuhakikisha Dunia inakua salama kwa viumbe wote wanaoishi, hakuna budi kutekeleza kikamilifu makubaliano mbalimbali ya kimataifa ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira yaliofanyika maeneo mbalimbali duniani kama vile Rio de Jeneiro, Paris, Kyoto pamoja na Glasgow. 


Amesema kinachohitajika ni utayari wa kisiasa pamoja na jitihada za pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinasababishwa na shughuli za binadamu.

Aidha, Makamu wa Rais amesema Tanzania imefanya jitihada mbalimbali katika kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kulinda misitu ya asili pamoja na juhudi za kitaifa za upandaji miti huku ikienda sambamba na kuhifadhi kilometa za mraba  307,800 ambazo ni sawa na asilimia 32.5  ya eneo lote la nchi kwa ajili ya Hifadhi za Taifa pamoja na misitu.

Makamu wa Rais amewakaribisha Wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania katika teknolojia rafiki kwa mazingira ikiwemo teknolojia zinazoweza kubadili taka kuwa nishati ya gesi na mbolea. Pia amewaalika watafiti kutoka mataifa yalioendelea kushirikiana na makampuni pamoja na watafiti wa ndani nchini Tanzania kwa kuendeleza teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira katika kutumia nishati ya jua na upepo iliopo nchini Tanzania.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema pamoja na Tanzania kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira bado suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele na mataifa yote kwani juhudi za Tanzania pekee hazitoweza kukabiliana na changamoto hiyo duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi