Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuacha tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu majumbani na kuwakosesha haki ya kupata elimu.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Amesema ni vema watoto hao wakapata elimu ili kuweza kutumia vipaji walivyonavyo kwani serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia ikiwemo ya shule jumuishi.
Makamu wa Rais amesema Rasilimaliwatu ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini ambapo elimu bora ndiyo inayowezesha uendelezaji wa rasilimali watu ili kuchangia kikamilifu katika kujenga Taifa na kuleta maendeleo kwa ujumla. Amesema sekta ya elimu ni kipaumbele cha Serikali zote mbili zinazoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kujenga jamii iliyoelimika na yenye maarifa muhimu.
Aidha, Makamu wa Rais ameongeza kwamba katika Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni vema kujivunia hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika sekta mbalimbali hususani elimu kama vile kuongezeka na kuboreshwa kwa miundombinu ya elimu katika ngazi zote, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kutoka 25,432 mwaka 1964 hadi kufikia wanafunzi 592,781 mwaka 2023. Mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuongezeka kwa Vyuo vinavyotoa elimu ya juu ambapo hivi sasa vimefika 7 kutoka 0 Mwaka 1964 pamoja na ongezeko la uwekezaji katika elimu ya juu kutoka nje ya nchi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi wananchi kutambua jukumu la kulinda na kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kukemea vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na dhamira hiyo. Amewaasa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya kila mmoja na Taifa kwa ujumla pamoja na vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea ama kuleta utengano.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhammed Mussa amesema kukamilika kwa mradi huo ni jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ili kuhakikisha elimu inapatikana katika mazingira mazuri. amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kufanya mapinduzi makubwa ya kielimu ambapo yanajumuisha uboreshaji wa miundombinu, kuongeza maslahi ya walimu pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa katika vituo vya kutolea elimu.
Amesema katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imefikia lengo la asilimia 150 katika utekelezaji wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu.