Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa washiriki wa Kongamano la lugha za asili kujielekeza katika kupanga mikakati itakayohakikisha Kiswahili na lugha nyingine za asili zinapata fursa katika uchumi wa kidijiti ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo.Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Four Points by Sheraton jijini Dar es salaam.
Amesema kongamano hilo linapaswa kuangazia namna ambavyo Kiswahili pamoja na lugha nyingine za asili za Afrika zitakavyotumika kuendeleza teknolojia za asili, kuchochea uvumbuzi, uwekezaji na kukua kwa diplomasia.Aidha, Makamu wa Rais amesema kongamano hilo linapaswa kusaidia kuonesha fursa zilizopo katika matumizi ya lugha za asili ili kuwafanya vijana kujipatia stadi na maarifa mbalimbali katika kujiandaa kwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia ndani na nje ya bara la Afrika.
Makamu wa Rais amesema kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kumepanua wigo wa matumizi ya Kiswahili na kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kiutamaduni. Amesema Kongamano hilo ni muhimu kubeba jukumu kubwa la kuibua fursa zaidi na kuendeleza historia ndefu ya Kiswahili katika kujenga uhusiano kati ya watu wa tamaduni, lugha na misingi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Amesema Katika muktadha wa ukuaji na maendeleo ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi lugha nyingine za asili, tamaduni na mifumo ya maarifa asili, katika Afrika Mashariki na Kati, wafanyabiashara wadogo na wanaoinukia “Wamachinga” wametoa mchango ambao hauna budi kutambuliwa na kuthaminiwa. Amesema lipo hitaji la kufanya utafiti wa kina ili kuona jinsi nchi za Kiafrika zinavyoweza kuendeleza mifumo inayozingatia ushiriki wa vijana na makundi kama ya wafanyabiashara waliojiajiri katika diplomasia ya kiuchumi na kukuza biashara.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika kukuza lugha ya Kiswahili ambapo inalenga kuifanya lugha hiyo kuendelea kuleta umoja, amani na kuvumiliana katika bara zima la Afrika. Amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendelea kushirikiana na Vyuo na Taasisi za nje katika kukuza Kiswahili na kuendeleza diplomasia ya kiutamaduni.Kongamano hilo limehudhuriwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joackim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, Wanadiplomasia, Watunga sera, Wafanyabiashara na wenye Viwanda, Viongozi wa Dini, Wanataaluma na Wakuu wa Taasisi za Utafiti, Vijana, Wanawake na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kiraia. Kongamano limeandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kwazulu Natal cha Afrika Kusini.