Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa Mgeni Rasmi Kilele Maadhimisho Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
Apr 05, 2024
Majaliwa Mgeni Rasmi Kilele Maadhimisho Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amefungua kikao cha maandalizi ya Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huwa inaadhimishwa Mei 3, kila mwaka na mwaka huu 2024 yatafanyika jijini Dodoma na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Na Georgina Misama, Maelezo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Mei 03, ambapo kwa Tanzania siku hiyo itaadhimishwa katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza na kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo pamoja na Waandishi wa Habari leo Aprili 05, 2024, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema maadhimisho hayo yatazinduliwa na Waziri mwenye dhamana Mhe. Nape Nnauye ambaye atazindua kliniki ya sheria kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, ambapo Mei 02, 2024 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Aksoni atakuwa mgeni rasmi katika shughuli mbalimbali zikiwemo semina, warsha, kongamano na maonyesho kutoka kwa wadau wa habari.

“Kwa mwaka huu 2024, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) ndiye Mwenyekiti wa maadhimisho hayo Tanzania, ambapo takribani wageni 300 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kuhudhuria na kwamba madhumuni ya maadhimisho haya ni kupitia kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari duniani, kuangalia uandishi wa taarifa za mazingira na mabadiliko tabia nchi na namna ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Matinyi.

Alisema maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu katika kuibua changamoto za kisera pamoja na kuangalia namna ya uboreshaji wa mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari nchini na kwamba maazimio yote yatakayotolewa katika majadiliano yatakayofanyika kwenye maadhimisho hayo yatachukuliwa na serikali kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Aidha, Matinyi alitoa rai kwa wadau wote wa tasnia ya habari nchini kuenzi na kuheshimu dhamira ya kiongozi wa nchi Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara tu alipoingia madarakani alionyesha dhamira yake ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo wakiwemo waandishi wa habari.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu Sayansi na Teknolojia (UNESCO), Michel Toto alisema, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani inawaleta pamoja waandishi wa habari katika kutetea haki zao na kuibua utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi