*Azindua Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini
*Asema utashusha bei ya vyakula mijini
CHANGAMOTO ya usafiri nchini, hususan maeneo ya vijijini kuwa historia baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Amesema wakala huo utasaidia kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na kuwawezesha wananchi wengi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi, hivyo kukuza uchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 02, 2017) wakati akizindua wakala huo katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma.
“Wakala huu tunaouzindua leo utakuwa na manufaa makubwa kwa ustawi wa nchi yetu kwa kuongeza chachu ya uzalishaji mali mashambani kutokana na urahisi wa kufika sokoni,”
“Utashusha bei ya vyakula mijini na bidhaa za viwandani vijijini kutokana na gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani na bidhaa za viwandani kutoka mijini kupungua,”
Aidha, Waziri Mkuu amesema manufaa mengine ya wakala huo ni kuboresha na kubadili hali za kimaisha na kiuchumi kwa wananchi kwani watakuwa wanasafiri kwa muda mfupi.
Pia utawezesha maeneo mengi ya nchi kufikika kwa urahisi, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika ujenzi, ukarabati na utengenezaji wa miundombinu ya barabara ikiwemo ya rushwa katika utoaji wa zabuni.
Amesema jambo hilo halikubaliki hivyo, amewataka watendaji wa TARURA wahakikishe wanatokomeza vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwenye utoaji wa zabuni, zitolewe kwa watu wenye uwezo wa kufanyakazi.
Waziri Mkuu amesema changamoto nyingine ni usimamizi hafifu wa mikataba ya ujenzi, ambapo ameelekeza isimamiwe vizuri na iwe ya wazi na yenye kutekelezeka.
Akizungumzia vitendo vya baadhi ya viongozi wa Halmashauri kubadilisha matumizi fedha za barabara, ameagiza fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya barabara zitumike kama ilivyopangwa.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mheshimiwa George Simbachawene alisema TARURA ni muhimu kwa kuwa zinagusa wananchi moja kwa moja na ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi, hivyo kuinua uchumi wa Taifa wenye msingi imara.
“Barabara hizi zinachochea kilimo katika ngazi ya jamii, zinaboresha ufikaji kwenye huduma za kijamii kama afya, elimu, maji na masoko, hivyo kuliwezesha Taifa kuwa na jamii imara kiafya, kiakili na kiuchumi,”.
Kutokana na umuhimu wa mtandao wa barabara za Vijijini na Mijini, Mheshimiwa Simbachawene ameomba mgawanyo wa mapato ya Mfuko wa Barabara wa asilimia 70 kwa TANROADS na asilimia 30 kwa Halmashauri uangaliwe upya, ambapo Waziri Mkuu ameridhia.
Waziri Mkuu alisema “Naamini kwa kuanzishwa TARURA sasa hoja hii inajadilika, tumieni taratibu zilizopo ili maamuzi yaweze kufanyika,”.
Mtandao wa barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kilomita 108,942.2 ambao ni Zaidi ya nusu ya barabara za Kitaifa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
DODOMA.
JUMAPILI, JULAI 02, 2017