Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAKUKURU Jiridhisheni na Huduma Zinazotolewa kwa Wananchi - Majaliwa
Oct 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_36461" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , Oktoba 8, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti.[/caption]

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa TAKUKURU wajiridhishe huduma zinatolewa kwa wananchi bila ya rushwa, watakapobaini rushwa wachukue hatua.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wajiepushe na vitendo vya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika utendajikazi wao.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 8, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa JWTZ.

“Msiwalazimishe au kutengenezea mazingira ya kuomba rushwa kwa wananchi. Wananchi mkiona mnazungushwa katika kupatiwa huduma katoeni taarifa TAKUKURU.”

[caption id="attachment_36462" align="aligncenter" width="750"] Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo wakimsikiliza Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Oktoba 8, 2018.[/caption]

Waziri Mkuu amesema “tabia ya njoo kesho njoo kesho haikubaliki katika Serikali hii. Serikali haitaki mtumishi mzembe anayedharau wananchi, fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zenu.”

Amesema Rais Dkt. John Magufuli anataka kila Mtanzania afikiwe na huduma za jamii bila ya ubaguzi wa aina yoyote, mtumshi atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake hatakuwa na nafasi Serikalini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Bi. Wende Ng’ahara awahamishe maafisa kilimo na kuwapeleka vijijini ili wakawahudumie wananchi.

Amesema maafisa kilimo wanaotakiwa kuwepo wilayani ni wawili tu, Afisa Kilimo wa wilaya pamoja na afisa kilimo anayeshughulikia mazao ya mbogamboga, wengine wanatakiwa kupelekwa vijijini kwa ajili ya kuhudumia wananchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Bibi Saada Malunde na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Wende wahakikishe wakuu wa idara wanakwenda vijijini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Wanatakiwa kwenda siku nne kwa wiki.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, OKTOBA 8, 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi