Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa Awataka Viongozi wa Serikali Kutekeleza Maagizo ya Rais Magufuli Katika Sekta ya Madini.
Jan 26, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Madini wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanatekeleza kwa haraka  maagizo yaliyotolewa na Rais John Pombe Magufuli ikiwemo kuanzisha masoko ya madini kwa lengo la kukabiliana na  changamoto za utoroshwaji  wa madini na migogoro kwa wachimbaji wadogo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini kwa lengo la kukabiliana na  changamoto hizo ili kuongeza tija katika sekta ya madini.

" Kwa muda mrefu Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kuhusu Sekta ya Madini kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu, sekta hii imekuwa na changamoto licha ya jitihada mbalimbali kuchukuliwa kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya madini" amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kutokana na umuhimu wa masoko hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi hao kuhakikisha kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini zinakamilika haraka kwa lengo la kusaidia wadau kupata soko la uhakika huku serikali ikinufaika na mrahaba na tozo mbalimbali.

"Nyote mtakubaliana nami kuwa kukamilika kwa  kanuni  hizo kutasaidia wananchi kupata masoko ya uhakika ya madini na wakati huo huo serikali kunufaika na mrahaba na tozo mbalimbali zinazotozwa kwa mujibu wa sheria" amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa kuwa  pindi kanuni hizo zitakapokuwa tayari zifikishwe kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuhakikisha makundi yote yanakuwa na uelewa wa kutosha na hatimae kuzisimamia kikamilifu kwa kushirikiana na Tume ya Madini.

"Ofisi ya Rais- TAMISEMI kupitia Wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala wa Mikoa wakishirikiana na Wizara pamoja na Tume ya Madini hamna budi kuhakikisha mnaandaa utaratibu ambao utawawezesha Wakurugenzi katika Halmashauri husika kutoa maoni yao katika kuanzisha masoko hayo na maoni hayo yawasilishwe Wizara ya Madini haraka kupitia Tume ya Madini ili yaweze kuzingatiwa kwenye kanuni zilizoandaliwa" ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewatakwa  Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la Ulinzi na Usalama wa masoko hayo  katika Mikoa yao.

"Serikali inategemea kuwepo na hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara, Wachimbaji na wananchi kwa ujumla usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo" amesisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo mbalimbali yaliyotolewa yenye lengo la kuboresha mchango wa sekta ya Madini nchini.

"Tanzania  ni moja kati ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu na vito ambapo kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini  hawana maeneo maalumu wanayoweza kufanyia biashara ya madini hali iliyochangia kuwepo kwa utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha Serikali mapato stahiki" ameeleza Waziri Biteko.

Waziri Biteko amesema kuwa , Ili kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati ya wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali ili kuandaa rasimu ya kanuni za kuanzisha na kusimamia masoko ya madini nchini.

Hivyo, amewaomba Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa, Maafisa Madini, Wakaazi wa Mikoa na Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kutimiza ndoto za muda mrefu za Wachimbaji wadogo, Wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote kwa ujumla kufikia malengo hayo na  kufanikisha sekta ya madini nchini

MWISHO

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi