Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Majaliwa Akutana na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi
Aug 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Mhe. Balozi Benedict Mashiba nyumbani kwa Waziri Mkuu leo Jijini Dar es Salaam

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Balozi Benedict Mashiba, ambapo amemtaka kuimarisha mahusiano baina ya nchi zote mbili.

Amekutana na Balozi Mashiba leo (Jumatano, Agosti 16, 2017) katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam, ambapo amemtaka balozi huyo kuhakikisha anaboresha shughuli za Kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi.

Pia Waziri Mkuu amemtaka Balozi huyo kuhakikisha anatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ukiwemo mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususan katika sekta ya viwanda.

Waziri Mkuu amesema licha ya kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii pia amemtaka kuboresha biashara baina ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli mbili za mizigo za Mv. Ruvuma na Mv. Njombe alizozizindua hivi karibuni.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amemtaka Balozi Mashiba kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio nchini Malawi na kuwasisiza kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Pia kuwaunganisha pamoja na kuwashauri waje kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Balozi Mashiba amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 

JUMATANO, AGOSTI 16, 2017.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi