Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maeneo Yaliyomegwa Kwenye Hifadhi Yapangiwe Mpango wa Matumizi ya Ardhi
Oct 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ametaka maeneo yanayomegwa kwa ajili ya kupatiwa wananchi waliovamia hifadhi yapangiwe mpango wa matumizi ya ardhi na kutolewa hati kwa wamiliki wake.

Dkt. mabula alitoa kauli hiyo Oktoba 27, 2022 katika Kijiji cha Mpanga kilichopo Wilaya ya Wanging'ombe wakati timu ya mawaziri nane wa wizara za kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea Mkoa wa Njombe ikiwa ni  mfululizo wa ziara zake kwenye Mikoa ya Tanzania Bara.

Kijiji cha Mpanga ni moja ya vijiji 11 vilivyopo katika Wilaya ya Wanging'ombe na Makete mkoani Njombe ambavyo vimemegewa eneo kutoka Hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.

Dkt. Mabula alisema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeridhia baadhi ya vijiji kwenye Mkoa wa Njombe kubaki maeneo ya hifadhi za Mapori ya Akiba ingawa wananchi wake waliingia bila ridhaa ya serikali.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, ili kuondokana na migogoro ya ardhi vijiji vilivyomegewa maeneo vitapimwa na kumilikishwa ili wamiliki kujua mipaka sambamba na kuweza kutumia hati kukopa fedha benki na fedha kutumika kuboresha shamba au mifugo.

"Kinachofanyika hapa siyo tu kutoa maeneo, eneo linatolewa lakini liwekewe mpango mzuri na endelevu ili kuona jinsi gani mnaweza kutumia ardhi mliyopewa kwa faida na kwa sababu tunaongezeka basi mpango uwe mzuri na endelevu" alisema Dkt Mabula.

Amebainisha kuwa, ni lazima maeneo yanayopangwa yaainishwe matumizi yake kama vile maeneo ya akiba, hifadhi, makazi na uwekezaji na kutaka wakati wa utekelezaji wataalamu wazingatie mpango wa matumizi katika maeneo hayo.

Timu ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ambayo inashughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 imemaliza ziara yake katika Mkoa wa Njombe ukiwa ni mkoa wa 22 kati ya 26 ya Tanzania Bara na inaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Ruvuma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi