Idara ya Habari - MAELEZO imekusanya jumla ya shilingi 354,190,750 sawa na asilimia 199 katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hayo leo Mei 20, 2022, bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/23 ya wizara hiyo.
"Idara ya Habari - MAELEZO ilikadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi 178,017,222 kutokana na mauzo ya picha za viongozi Wakuu wa Nchi na picha ya Baba wa Taifa, vitambulisho, machapisho na ada ya mwaka ya magazeti. Hadi kufikia Aprili 30, 2022, Idara imekusanya jumla ya shilingi 354,190,750 ambayo ni sawa na asilimia 199," alifafanunua Nnauye.
Aliendelea kusema kuwa, kuvuka lengo kwa makusanyo ya idara hiyo kumetokana na kuuzwa kwa wingi kwa picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hasaan baada ya kuapishwa.
Nnauye aliendelea kusema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23, wizara kupitia Idara ya Habari-MAELEZO imejipanga kutekeleza majukumu mbalimbali kama vile kukusanya taarifa na kuisemea Serikali kuhusu utekelezaji wa sera, mikakati, miradi na programu inazozitekeleza.
Majukumu mengine ni kuazisha Bodi ya Ithibati ya wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari pamoja na kufanya mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 ili kuifanya iendane na mabadiliko katika sekta ya habari.
Vilevile, Idara itafanya mapitio ya baadhi ya vifungu katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017, kuchapa na kutoa leseni za magazeti na vitambulisho vya Waandishi wa Habari pamoja na kutoa miongozo na kufanya tathmini ya utoaji taarifa kwa umma kwa kila taasisi.
Katika mwaka wa fedha 2022/23, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 282,056,786,000.00.