Vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamejitokeza kwa wingi katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam, kushiriki zoezi la usajili na usaili wa madereva bodaboda 500 wanaotarajiwa kwenda kufanya kazi katika Falme za Kiarabu (UAE).
Zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Serikali ya kuwaunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kupitia mifumo rasmi, inayolenga kuhakikisha ulinzi wa haki, maslahi na usalama wa wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya Tanzania.
Akizungumza Februari 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Jane Sorogo, amesema vijana wengi wamejitokeza kushiriki usaili huo, hali inayoonesha mwitikio chanya kwa fursa za ajira za kimataifa.

Amesema baada ya kukamilika kwa usaili jijini Dar es Salaam, mchakato huo utaendelea katika mikoa ya Tanga na Mwanza ili kutoa nafasi kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali kushiriki.
“Vijana watakaofaulu usaili huo wataelekea katika vituo vya kazi Falme za Kiarabu (UAE). Nawasihi vijana kuchangamkia fursa za ajira za nje ya nchi zinazojitokeza, kwani ni fursa ambazo nyuma yake kuna Serikali inayosimamia mchakato mzima,” amesema Sorogo.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliojitokeza kuwania nafasi hizo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kufungua milango ya ajira nje ya nchi kwa vijana wa Kitanzania. Wamesema fursa hiyo itawasaidia kuinua kipato chao na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao.

Aidha, wameiomba Serikali kuendelea kuwasimamia na kulinda maslahi yao wanapokuwa nje ya nchi, huku wakihamasisha vijana wenzao kujitokeza kwa wingi pale fursa kama hizo zinapotangazwa rasmi kupitia vyombo vya Serikali.
Mpango huo unaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana kwa kupanua wigo wa masoko ya ajira kimataifa kupitia utaratibu ulio rasmi na salama.