Na Daudi Manongi-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Madereva wa Bajaji na Bodaboda kuacha kutumika katika vitendo vya uhalifu
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo Julai 24, 2022 alipopiga simu wakati wa Kongamano la Ushiriki wa Waendesha Bodaboda na Bajaji katika kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka 2022.
“Nyinyi ni Maafisa Usafirishaji wa Taifa na ni Sekta
muhimu sana katika Taifa hili, lakini baadhi yenu wanatumika vibaya, bodaboda zinapita kukwapua mizigo na pochi za wanawake kwa hiyo katika maeneo yao wakataze hilo na wakatae kutumika kwa ujambazi,” amesema Mhe. Rais katika Kongamano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Aidha, amewataka waendesha Bodaboda na Bajaji hao kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 nchini kote.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema hawatafungia vyombo vyote vya usafiri kwa kosa moja la mfanyabiashara mmoja wa Bajaji au Bodaboda.
“Ni lazima tuelewa kwamba hii ni biashara ambayo watu wanaishi, wanaendesha familia zao, kuna wazazi wanapata matibabu kwa ajili ya biashara hii, kuna zaka na sadaka na michango kwa sababu ya biashara hii, kwa hiyo lazima tuheshimu biashara hii ” ameongeza
Aidha, amewataka waendesha Bajaji na Bodaboda kuchangia katika Mfuko wa NSSF, kukata Bima ya Afya na kuondoka katika mikopo yenye masharti magumu na kwenda kwenye mabenki.