Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo, mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifuani na kupeleka kwenye mishipa ya damu ya miguuni (Axillobifemoral Bypass Graft Surgery).
Upasuaji huo ni wa kwanza kufanyika hapa nchini ambapo mgonjwa alikuwa na tatizo la kupata maumivu makali maeneo ya miguuni, mapaja na sehemu ya kukalia kwa muda wa miezi nane baada ya uchunguzi ikagundulika mshipa wake mkubwa wa damu (Abdominal Aorta) umeziba kabisa na hivyo kushindwa kupeleka damu kwenye miguu (Aortoilliac Occlusion Disease) damu ilikuwa inapelekwa kupitia mishipa midogo (Collaterals).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana jijini Dar es Salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, mishipa ya damu na kifua wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph alisema walimpokea mgonjwa huyo wiki iliyopita kutoka Hospitali ya Mnazi mmoja iliyopo Visiwani Zanzibar.
Dkt. Alex alisema upasuaji wa aina hiyo haujawahi kuufanya hivyo basi baada ya majadiliano ya jopo la madaktari bingwa na kushauriana na mgonjwa waliona waufanye kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa mgonjwa kupona na kutoka katika maumivu makali aliyokuwa nayo.
“Upasuaji tulioufanya ni wa kupandikiza mrija bandia wa damu na kuukwepesha eneo ambalo limeziba. Tuliweka mrija kama mshipa bandia wa damu kutoka kwenye mshipa wa damu wa kifua upande wa kushoto na kuupitisha pembeni ya kifua na tumbo mpaka kwenye mguu wa kushoto na kisha kuelekea mguu wa kulia”,.
“Baada ya kufanya upasuaji huo hivi sasa miguu yote miwili inapata damu ambayo inatoka moja kwa moja kwenye mshipa wa damu wa kifuani kwani tuliikwepesha eneo la tumboni ambalo mshipa umeziba”, alisema Dkt. Alex.
Dkt. Alex alisema hii ni faraja kwao kwani hivi sasa huduma za matibabu ya magonjwa kama hayo pamoja na mengine ya matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu zinapatikana hapa nchini na hakuna haja ya kusafiri kwenda kutibiwa nje ya nchi ambako gharama ni kubwa kati ya milioni 15 hadi 20 wakati hapa nchini huduma inapatikana kwa gharama naafuu.
Kwa upande wake Mama Fatma Khamis ambaye alifanyiwa upasuaji huo alisema kwa muda wa miezi nane iliyopita miguu ilikuwa inamuuma baadaye akapata kidonda ambacho hakikupona hata baada ya kwenda Hospitali. Baadaye akaenda kwa daktari wa mifupa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar ambapo baada ya kufanyiwa vipimo akaambiwa anatatizo la damu kuganda na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) iliyopo Dar es Salaam kwani hospitali hiyo haikuwa na uwezo wa kumtibu.
“Baada ya kufika JKCI nilifanyiwa vipimo na kuambiwa mshipa mkubwa wa damu haupitishi damu katika miguu na hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu niliambiwa katika upasuaji huo naweza kupona au la na hivyo kupewa fomu za kusaini nikasaini.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji niko vizuri kama unavyoniona naweza kusimama na kutembea vizuri maumivu ya miguu yamepungua tofauti na nilivyokuwa mwanzo”, alisema Mama Fatma.
Aliwashauri watanzania wenye matatizo kama hayo wasipate tabu na wasihangaike kwenda kutibiwa nje ya nchi kwani hapa nyumbani ambapo ni karibu huduma hiyo inapatikana.
“Ninaishukuru sana Serikali yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunilipia gharama za matibabu haya na sasa hivi nimefanikiwa niko vizuri”, alishukuru Mama Fatma.