Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maboresho ya Bandari Nchini Yapaisha Mapato ya Serikali
Feb 01, 2026
Maboresho ya Bandari Nchini Yapaisha Mapato ya Serikali
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mafanikio ndani ya siku 100 za Serikali ya awamu ya Sita, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Na Aron Msigwa - MAELEZO

Serikali imesema itaendelea kuimarisha usalama na huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya maziwa makuu ili kukuza uchumi na ushiriki wa wananchi katika shughuli za usafirishai wa mizigo na biashara ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 1, 2026 na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuelezea mfanikio yaliyopatikana katika sekta ya uchukuzi ndani ya kipindi cha siku 100 za muhula wa pili wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Profesa Mbarawa amesema katika kuendeleza mkakati wa kuimarisha usafiri majini, Serikali imekamilisha ujenzi wa Meli ya MV New Mwanza katika Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400 ambayo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Januari 23, 2026

Amesema meli hiyo imeanza kutoa huduma za kisasa za usafiri wa abiria na mizigo kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Mikoa jirani pia kuhudumia wafanyabiashara wa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jambo ambalo limeongeza usalama na ufanisi wa usafiri ndani ya Ziwa Victoria

Kwa upande wa maziwa makuu, Profesa Mbarawa amesema Wizara imekamilisha ujenzi wa Meli mbili (2) za kisasa za mizigo katika Ziwa Tanganyika kati ya meli nne (4) zinazojengwa kwa ubia kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na sekta binafsi kwa mfumo PPP, zenye uwezo wa kubeba tani 2,000 kila moja ambazo zitaboresha biashara na usafirishaji kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Serikali imewezesha kuanza kwa safari za Meli ya MT Sangara baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ambapo sasa inafanya safari za kibiashara za kusafirisha shehena ya mafuta kati ya Kigoma na Kalemie nchini DRC tangu mwezi Juni, 2025.

Katika eneo la Ziwa Nyasa, Profesa Mbarawa amesema, Serikali kupitia TPA inaendelea kutekekeza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay unaohusisha ujenzi wa gati ya kuhudumia shehena ya magari (RO-RO) na meli, jengo la utawala, uzio, barabara, jengo la kuhifadhia mizigo pamoja na Jengo la Abiria ambapo mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi