Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maboresho Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma Yaleta Mapinduzi Sekta ya Zabuni
Feb 25, 2026
Maboresho Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma Yaleta Mapinduzi Sekta ya Zabuni
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Miradi ya Maendeleo na fursa kwa Vijana, katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma.
Na Na. Baraka Messa- MAELEZO

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema maboresho yaliyofanyika kupitia Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya ununuzi na ugavi nchini, hususan kwa kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya zabuni za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 25, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, amesema sheria hiyo imelenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa rufaa za zabuni.

Amesema kuwa mwaka 2023 Serikali ilitunga upya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, ikifuatiwa na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 pamoja na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2025. Hatua hizo, amesema, zimelenga kuimarisha mfumo wa kisheria na kiutendaji katika sekta ya ununuzi na ugavi.

“Maboresho haya yameimarisha na kuleta ufanisi katika sekta ya Ununuzi na Ugavi kwa kuunganisha maeneo ambayo kitaalamu yanapaswa kuwa pamoja,” amesema Sando.

Ameongeza kuwa kupitia maboresho hayo muda wa kuwasilisha malalamiko umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano pia muda wa Afisa Masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni umepunguzwa kutoka siku saba hadi siku tano za kazi.

Aidha, Sado amesema muda wa kuwasilisha rufaa PPAA umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano, huku muda wa Mamlaka ya Rufani kusikiliza na kutolea maamuzi malalamiko au rufaa ukipunguzwa kutoka siku 45 hadi siku 40 ili kuharakisha utoaji wa haki, kupunguza ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza tija katika matumizi ya fedha za umma.

Pia amesema kuwekwa kwa muda maalum wa kusikiliza na kutolea maamuzi rufaa kumeondoa changamoto ya ucheleweshaji iliyokuwa ikilalamikiwa na wadau wa zabuni.

Katika hatua nyingine Sando amesema kutokana na maboresho hayo, PPAA inatarajia kuongezeka kwa imani ya wazabuni katika mfumo wa ununuzi wa umma pamoja na kuimarika kwa utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi