Na Mwandishi wetu-MAELEZO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Maafisa Elimu Mkoa na Wilaya kutekeleza kwa umakini Mwongozo wa kufundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Ummy ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo kwa wawezeshaji ya kuwapitisha kwenye mwongozo wa kufundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Amesema kuwa, ili kuweza kupambana na rushwa nchini ni vyema kuwashirikisha watanzania kwa ujumla ikiwemo vijana wadogo waliopo mashuleni .
Aidha, Waziri Ummy ameeleza kuwa maamuzi yakushirikisha skauti katika mapambano dhidi ya rushwa ina umuhimu kwa Ustawi wa Jamii kwa kuwa vijana hao watakuwa na uwekezaji madhubuti kuhusu mapambano dhidi ya rushwa tangu wakiwa wadogo.
“Takribani jumla ya vijana 13,700,000 wa shule za sekomdari na msingi waliopo mashuleni wataguswa na mkakati huu kupitia skauti hivyo maamuzi ya kuwatumia skauti ni muhimu kwa ustawi wa taifa letu”, amesisitiza Ummy.
Vilevile, Ummy ameelekeza mamlaka ya shule za msingi na sekondari zilizopo chini ya TAMISEMI kutoa fursa ya mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa katika matukio mbalimbali yanayotokea mashuleni.
Hata hivyo, Waziri Ummy ametoa rai kwa Maafisa Elimu kuandaa mpango kazi na ikiwezekana kuingizwa kwenye bajeti masuala yanayohusu skauti ili kuweza kuwaendeleza katika maeneo yao.
Mbali na hayo, ametoa rai kwa wawezeshaji waliopata mafunzo hayo kusimamia kwa umakini na kuuelewa mwongozo huo ili kuweza kutumika kwa lengo lililokusudiwa la kuelimisha vijana wa skauti ili kuichukia rushwa na kushiriki kuzuia na kupambana nayo ingali wakiwa vijana wadogo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Neema Mwakalyelye amesema kuwa lengo kuu la mkakati huo ni kuelimisha vijana wa skauti kuichukia rushwa na kushiriki kuzuia na kupambana nayo ingali wakiwa vijana wadogo.
Pia ametoa rai kwa wawezeshaji hao kuyaishi yale waliyokubaliana ili kuweza kuwafundisha vijana wa skauti namna ya kuendeleza gurudumu hilo la kuzuia na kupambana na rushwa nchini
Aidha, ameongeza kuwa mwongozo huo umebeba mambo yanayohusu mbinu mbalimbali za ufundishaji na nadharia za mada kuhusu rushwa ikiwa na madhumuni ya kuwajenga vijana kimaadili, misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.
Nae, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza amesema kuwa ushirikiano kutoka kwa maafisa elimu nchini utasaidia kutimiza lengo la TAKUKURU na Skauti la kufundisha vijana kuhusu kuzuia na kupambana rushwa nchini.
“Vita hii ya kuzuia na kupambana na rushwa tukipigana pamoja nchi yetu itakuwa mahali salama dhini ya rushwa hivyo tunahitaji kushirikiana kwa dhati ili kuweza kutimiza lile lengo tulilojiwekea”, amesisitiza Mwantumu.
Takribani washiriki 105 wamenufaika na mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tatu kwa makundi yakiwezeshwa kwa ushirikiano wa Chama cha Skauti Nchini, TAMISEMI, Shirika lisilo la Kiserikali la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) pamoja na TAKUKURU.