Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Maadhimisho Siku ya Mazingira iwe Chachu ya Kuongeza Kasi ya Jamii Kushiriki Shughuli za Kuhifadhi na Kutunza Mazingira Nchini – Waziri Dkt. Jafo
May 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa wananchi kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaendelee kuwa chachu ya kuongeza kasi ya uhamasishaji wa jamii kushiriki shughuli za kuhifadhi na kutunza mazingira nchini. 

Waziri Dkt. Jafo ametoa rai hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Juni 5, kila mwaka ambapo kwa mwaka huu yatafanyika jijini Stockholm nchini Uswisi yakiwa na kaulimbiu ya “Only One Earth”, na kwa Tanzania yatafanyika jijini Dodoma yakiwa na kaulimbiu ya ”Tanzania ni moja tu: Tutunze Mazingira”. 

“Kaulimbiu hii inatuhamasisha sisi wananchi kwa pamoja kila mmoja katika shughuli zake za kila siku kutunza mazingira ya nchi yetu ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa mahali salama pa kuishi kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo, natoa wito kwa Watanzania wote kufahamu kuwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni jukumu letu sote, kila mmoja kwa nafasi yake kwa kuwa tusipotunza mazingira yetu sisi wenyewe, hakuna mtu yoyote kutoka kwingine atatufanyia kazi hiyo”, alisema Waziri Dkt. Jafo. 

Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa, maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali na umuhimu wa kuhifadhi mazingira katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuelimisha wananchi kuhusu: kushiriki shughuli za kuhifadhi na usimamizi mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira, matumizi ya mbinu mbalimbali za kuhimili na kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi, kudhibiti kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, upotevu wa bioanuai, uharibifu wa tabaka la ozoni, pamoja na udhibiti wa shughuli nyingine zisizoendelevu zinaweza kuchangia uchafuzi na uharibifu wa mazingira. 

Akizungumza kuhusu utekelezji wa maadhimisho hayo, Waziri Dkt. Jafo amefafanua kuwa siku ya kilele cha maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan atahutubia wadau wa mazingira na Taifa kwa ujumla kupitia Vyombo vya Habari, pia atazindua Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira. 

Aidha, kilele cha maadhimisho hayo kitatanguliwa na Wiki ya Mazingira inayoanza tarehe 28 Mei – 4 Juni 2022 ambapo shughuli mbalimbali za hifadhi na usafi wa mazingira zitafanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma zikihusisha wananchi, taasisi, mashule, vyuo na viongozi mbalimbali. 

Vile vile, maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira ya mwaka huu yatahusisha maonesho ya wadau ya shughuli mbalimbali za kuhifadhi Mazingira yatakayo anza tarehe 1 – 5 Juni 2022 katika viwanja vilivyopo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma. 

Waziri Dkt. Jafo ametoa wito kwa Mikoa yote kutumia Redio za Halmashauri za mikoa kuhamasishana na kuelimisha jamii masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira ikiwemo kutumia nishati mbadala wa mkaa majiko bunifu pamoja na kutumia njia sahihi za kuhifadhi taka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi