Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda amesema Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowassa alikuwa kiongozi aliyekuwa anajua kusimamia kile alichokuwa anataka kifanyike.
Mhe. Mizengo amesema hayo leo Kijiji cha Ngarash wilayani Monduli leo Februari 16, 2024 wakati wa ibada ya kumuuga Hayati Lowassa iliyofanyika kijijini hapo, ambaoo ni nyumbani kwa kiongozi huyo.
“Alipokuwa Waziri Mkuu nilipata nafasi ya kufanya kazi naye, alikuwa ni kiongozi aliyekuwa anajua kusimamia kile alichokuwa anataka kifanyike, na alikuwa hana utani katika hilo,” amesema Mhe. Mizengo.
Ameendelea kusema kuwa, na hata unapokamilisha kazi fulani alikuwa akihamasisha kupeana hongera badala ya kupeana pole, kwani alikuwa anaamini unapomaliza jukumu fulani unastahili kupewa hongera kwa kukamilisha jambo hilo, na sio kupewa pole.
Mhe. Pinda amesema Hayati Lowassa amefanya mambo mengi ya kuigwa akiwa mtumishi na mtendaji wa serikali, hivyo amewataka Watanzania kuiga yale mema aliyoyafanya kiongozi huyo na kuyaendeleza.
Hayati Edward Lowassa anatarajiwa kuzikwa Februari 17, 2024 nyumbani kwake Kijiji cha Ngarash kilichopo wilayani Mondulu mkoani Arusha, ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atawaongoza Watanzania katika mazishi ya kiongozi huyo.