Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Tixon Nzunda ametoa wito kwa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuimarisha mifumo ya utafiti na ushauri kwa wafugaji,sambamba na kuongeza ubunifu kwa kuanzisha huduma mtandao zenye kuwaunganisha pamoja na wafugaji, wadau wa sekta ya mifugo na taasisi zingine za Umma na binafsi.
Nzunda ametoa wito huo mkoani Morogoro wakati akizungumza na Bodi ya wakala hiyo na Maafisa wasimamizi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya mifugo kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
"Anzisheni mifumo imara ya usimamizi na uwajibikaji, huu utendaji wa kuamka asubuhi unaenda kazini kama kawaida, umepitwa na wakati, unachelewesha maendeleo, kwa sasa tuanze kupimana kwa Mikataba ya utendaji kazi ili tuanze kuona utendaji wa kila mmoja wetu jinsi anavyotekeleza majukumu aliyopewa, kama umefanikiwa, sawa, na kama amekwama tatizo ni nini mpaka umekwama? hii itatupa nafasi ya kuhoji kama unastahili kuendelea na nafasi uliyonayo. alisema Nzunda"
Nzunda amesisitiza kuwa Serikali inahitaji kuona matokeo chanya kupitia Sekta ya Mifugo kwa kuimarisha na kusogeza huduma kwa wananchi ikiwemo kuendelea kupanua wigo wa huduma za ugani kwa wafugaji ili kuondokana na ufugaji wa mazoea usioleta tija kwa wafugaji walio wengi.
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo ni muhimu itekeleze jukumu la kuwafikia wafugaji kwa kutumia rasilimali kidogo waliyonayo ili kuleta matokeo makubwa.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala hiyo, Prof. Malongo Mulozi, amesema kuwa LITA wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa usafiri wa kuwapeleka wanafunzi katika masomo ya vitendo pamoja na kuwafikia wafugaji.
Aidha, ametaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa miundombinu ya kufundishia na uhaba wa nyumba za watumishi ambapo alibainisha kuwa pindi fedha itakapopatikana ukarabati na ujenzi wa nyumba hizo utaanza mara moja.
Vile Vile Prof. Mlozi amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa changamoto hizo, moja ya mikakati ya Taasisi hiyo ni kuzalisha na kuandaa vijana wenye uwezo wa kujiajiri kupitia Sekta ya Mifugo na kwamba kila kituo kina mradi wake wa mapato kulingana na hali ya mazingira kilipo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa majukumu makubwa ya Taasisi yake ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kutoa huduma za ushauri wa kitalaam wa Mifugo, kufanya tafiti na tathimini pamoja na kuzalisha na kutunza mifugo ya kufundishia.
Dkt. Mwambene amesema kuwa, kwa sasa vyuo hivyo vina wanafunzi zaidi ya 4,000 ukilinganisha na wanafunzi 700 waliokuwepo wakati wanaanza mafunzo hayo miaka kumi iliyopita, na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) imeendelea kuhimiza kufanyika maboresho katika miundombinu ikiwa ni pamoja na kusimamia ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika vyuo hivyo.
Pia Dkt. Mwambene ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuingia ubia na wakala hiyo ili kusaidia uwekezaji wa mafunzo kwa wanafunzi hao.
Mazungumzo baina ya Nzunda na Watendaji wa Wakala hiyo yalienda sambamba na makabidhiano ya magari mawili aina ya "Toyota Double cabin" kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa taasisi hiyo.