Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Lindi Watakiwa Kushiriki Katika Zoezi la Umezaji Kingatiba
Jun 28, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na WAMJW-Lindi

Wakazi wa Lindi na vitongoji vyake wametakiwa kushiriki katika kampeni ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa kumeza kingatiba za kutokomeza magonjwa hayo pamoja na kutunza mazingira kwa kuondoa mazalia ya mbu waenezao magonjwa hayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa kambi ya upasuaji wa Mabusha na Ngirikokoto (Henia) unaofanyika mkoani Lindi.

"Wakazi wa Lindi na Vitongoji vyake tunatakiwa kushiriki katika zoezi la kumeza dawa za kukinga magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele pamoja na kufanya usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu", alisema Dkt. Ndugulile

Aidha, Dkt. Ndugulile amewataka wananchi wa Lindi kuondoa dhana potofu ya kuwa kila mwenye mabusha au ngirimaji basi atakuwa amerogwa ila ajue ugonjwa huo unasababishwa na vimelea vinavyotokana na mbu na kuzingatia umezaji wa dawa hizo.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuhakikisha wanapambana kutokomeza ugonjwa huo Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Utafiti ya uchimbani mafuta na gesi ya Statoil wamepata fedha za kuwafanyia upasuaji wagonjwa 200 wa mabusha na ngirikokoto kwa awamu ya kwanza ya mwaka 2017 na wagonjwa 200 kwa awamu ya pili ya mwaka 2018.

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa wananchi wa Lindi wanatakiwa kutoa taarifa sehemu husika pindi wanapoambiwa kuwa dawa muhimu hakuna kwenye vituo vya afya vya Serikali kwani dawa hizo zipo kwa asilimia 90 Mkoani humo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bw. Ramadhani Kaswa amesema kuwa umezajii wa kingatiba ya magonjwa hayo umefikia asilimia 70 kwa mwaka 2016/2017.

Aidha, Bw. Kaswa amesema kuwa kutokana na zoezi la kuwatambua wagonjwa wenye mabusha na ngirikokoto wamejiandikisha wagonjwa 1294 kwa mkoa wa Lindi ikiwemo Manispaa ya Lindi wagonjwa 67, Wilaya ya Nachingwea wagonjwa 101, Halmashauri ya Lindi wagonjwa 633, Wilaya ya Liwale wagonjwa 387 na Wilaya ya Luongo wagonjwa 106.

Uzinduzi huo uliambatana na zoezi la kumeza Kingatiba za  magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo mabusha na matende,usubi,minyoo,trakoma( vikope) na vichocho.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi