Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ni Kuimarisha Udugu - Dkt. Mwinyi
Apr 26, 2024
Kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ni Kuimarisha Udugu - Dkt. Mwinyi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Na Jonas Kamaleki- Maelezo

Hatua iliyofanywa na viongozi wakuu waasisi wa taifa letu ya kuziunganisha iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa taifa moja la Tanzania, ilikuwa na dhamira ya kuimarisha udugu wa damu na wa kihistoria wa wananchi wa nchi hizi mbili.

"Tukiwa tunaadhimisha miaka 60 ya muungano, tuna wajibu wa kumshukuru Mungu kwa mafanikio makubwa ambayo nchi yetu imeyapata katika sekta mbalimbali na kuendelea kupata sifa na heshima kimataifa kutokana na muungano huu na kuwa nchi ya kupigiwa mfano kwa kudumu kwa muungano huu huku kukiwa na amani, umoja na mshikamano", alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Aliwashukuru viongozi wa awamu zilizopita kwa jitihada zao za kudumisha na kuendeleza malengo ya muungano wa Tanzania na kuzifanyia kazi changamoto za muungano, ni jambo la faraja na kutia moyo kuona changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi.

"Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar, ninawaahidi Watanzania wenzetu kuwa tutaendelea kuwa waumini wa dhati wa muungano wetu na tutahakikisha unadumu, unaendelea na unazidi kuimarika kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye", alisema Dkt.  Mwinyi.

Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema Muungano wa Tanzania, ni muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kuna sababu kubwa iliyotutoa Burundi kuja kujiunga nanyi kushiriki katika maadhimisho haya.

"Kabla ya wakoloni kufika kwetu, Waha, Wahangaza na Warundi walikuwa wandugu, Warundi na Watanzania walikuwa wakitembeleana. Mpaka wa Burundi na Tanzania umeletwa na mkoloni lakini mpaka sasa Watanzania wa Kigoma na Kagera huwezi kuwatofautisha na Warundi", alisema Rais Ndayishimiye.

Mpaka baina ya Burundi na Tanzania uliowekwa na wakoloni ulikuwa ni kwa ajili yao lakini kwa upande wetu, umoja umebaki imara. Furaha ya Watanzania ni furaha ya Warundi, tunawapongeza kwa kufikia miaka 60 ya muungano.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi