Na Tiganya Vincent - RS Tabora
Kongamano la fursa za biashara ambalo linaendeshwa na Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) limesaidia kutangaza maeneo yenye fursa za uwekezaji katika mikoa ambayo imefanyika na kuwezesha baadhi ya watu kuonyesha nia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Daily News na Habarileo, Tuma Abdallah wakati wa Mkutano na Kamati ya Maandalizi Kongamano hilo mkoani Tabora.
Alisema kupitia Waandishi wa Habari wao wamekuwa wakitangaza ndani na nje ya nchi fursa mbalimbali zinazopatikana katika eneo husika ambapo baadhi imeanza kupata maombi kutoka kwa wawekezaji.
Tuma alisema lengo ni kutaka mikoa itumie fursa walizonazo katika maeneo yao katika kuwaleta wakazi wake maendeleo na Mkoa kwa ujumla.
Alisema kupitia kongamano lililofanyika mkoani Geita, yamepelekea kupata maombi ya Wawekezaji kutoka nchini Uganda ambao wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika maeneo mbalimbali.
Tuma aliitaka Mikoa yote kuandaa maelezo ya maeneo ya uwekezaji ambayo Kampuni hiyo itasaidia kutangaza kwa nia ya kuwavutia wawekezaji.
Aidha alisema Kongamano hilo limekuwa likiwashirikisha Watendaji kutoka Shirika la Viwango Tanzania(TBS), Mamlaka ya Mapato, Mamlaka ya chakula na Dawa (TFDA) kwa ajili ya kutoa elimu ambayo itawasaidia wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kuzingatia ubora na viwango.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliiagiza Kamati ya Mkoa huo kuhakikisha ndani ya mwaka huu wanakamilisha maandalizi na zoezi hilo la kuendesha kongamano hilo linafanyika.
Alisema Tabora ina fursa nyingi za uwekezaji lakini bado hazijatangazwa vizuri kwa hiyo kongamano hilo linafanyika muda mzuri ambapo miundombinu ya barabara imefunguka na kuufanya mkoa huo kuwa mahali bora kwa ajili ya uwekezaji.