Kongamano la TEHAMA la Connect to Connect Kufanyika Nchini Septemba
Jul 25, 2022
Na
Jacquiline Mrisho
Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku amesema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na kampuni ya Extensia kutoka nchini Uingereza wamesaini makubaliano ya kuandaa kongamano la TEHAMA litakalofanyika nchini Septemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Munaku amesema kuwa kongamano hilo lilifanyika nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na kuendelea hadi mwaka 2015 ambapo wadau kutoka nchini na nje ya nchi walishiriki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza baada ya kusaini Mkataba wa Makubaliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza, Bw. Tariq Malik (kushoto) wenye lengo la kuandaa Kongamano litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi linalojulikana kama Connect To Connect leo Julai 25, 2022 jijini Dodoma.
“Mwaka 2016 hadi 2021 kongamano hili lilifanyika katika nchi zingine duniani, mwaka huu Septemba 7 na 8 litafanyika hapa nchini katika jiji la Dar es salaam ambapo tunatarajia takriban washiriki 300 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mashirika yanayosimamia mawasiliano Afrika na duniani yatashiriki” anasema Munaku.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza, Bw. Tariq Malik akizungumza wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba wa makubaliano baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tewknolojia ya Habari na Kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza leo Julai 25, 2022 jijini Dodoma
Alifafanua “lengo la kongamano hili ni kuongeza matumizi ya Mkongo wa Taifa na kuongeza ubunifu na uwekezaji katika masuala ya TEHAMA ili kuongeza ajira na mapato kwa Serikali sambamba na kutoa fursa kwa watu wengine waje kujifunza nchini”.
Picha ya pamoja ya baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Jim Yonazi (wa nne kushoto mstari wa mbele) na watendaji kutoka Kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw. Tariq Malik (wanne kulia mstari wa mbele kabla ya kusaini mkataba wa makubaliano baina ya Wizara na Kampuni hiyo wa kuandaa Kongamano litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi linalojulikana kama Connect To Connect leo Julai 25, 2022 jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa Mkongo wa Taifa ni nguzo muhimu ya kufikia Tanzania ya Kidijitali ambayo inalenga kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kikamilifu kuimarisha uwekezaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kujenga chuo cha TEHAMA nchini”, anasema Msigwa.