Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika Kuchagiza Matumizi Nishati Safi ya Kupikia
Oct 02, 2024
Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika Kuchagiza Matumizi Nishati Safi ya Kupikia
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Oktoba 02, 2024 jijini Dodoma kuhusu ufunguzi wa kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10).
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania (TGDC) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) imeandaa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) ambalo litachagiza adhma ya Serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kuanzia tarehe 21-27 Oktoba, 2024.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba ameyasema hayo leo Oktoba 02, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufunguzi wa kongamano hilo ambalo linatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango na kufungwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

 "Kongamano hili lina kaulimbiu inayosema, "Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na Upunguzaji wa Gesi ya Ukaa", kaulimbiu hii inasadifu adhma ya Serikali kupitia Rais wake Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia", amesema Mhandisi Mwangomba.

Mhandisi Mwangomba amesema kuwa washiriki wa kongamano hilo watafaidika kwa kupata elimu na maarifa, mtandao wa kitaaluma, fursa za biashara, ziara za mafunzo, ufahamu wa sera na masoko, kukuza uwezo na kupata maarifa ya kimataifa.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki takriban 1000 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Djibouti, Newzealand, Japan, Iceland, Marekani, Canada na Saudi Arabia.

Akizungumza kuhusu nishati ya jotoardhi, amesema kuwa nishati hiyo ni endelevu, salama na rafiki wa mazingira na ina faida nyingi ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kutoa umeme bila kuzalisha gesi chafu, kutoharibu mazingira na uwezo wa kutoa umeme kwa kiwango kikubwa.

"Kwa sasa TGDC imeainisha takriban maeneo 52 katika mikoa 16 nchini ambayo ina uwezo wa kuzalisha nishati ya umeme zaidi ya megawati 5,000 na nishati ya joto zaidi ya megawati 15,000. Kampuni inaendelea na miradi mitano ya kipaumbelea ambayo inalenga kuzalisha MW 200 za umeme." Amemalizia Mhandisi Mwangomba.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi