Kiwanda cha kuwekea mifumo ya upashwaji joto mafuta pamoja na plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba yatakayotumika kwenye mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kinatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Januari 2023.
Hayo yalielezwa tarehe 24 Julai, 2022 wakati Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba alipofika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora ili kukagua kazi zinazoendelea katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Baada ya kukagua kazi mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa ikiwemo ya kusafisha eneo na ujenzi wa kiwanda, Waziri wa Nishati aliwaasa Wakandarasi wazawa kuikamilisha kazi hiyo kwa weledi na viwango stahiki hali itakayofanya wailetee sifa Tanzania na kuaminika ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa, lengo la Serikali ni kukamilisha ujenzi wa kiwanda mwezi Desemba mwaka huu, hivyo matarajio ya Serikali kuwa Wakandarasi hao wazawa watatimiza lengo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Buriani alisema Serikali ya Mkoa huo itaendelea kuusimamia mradi huo na kueleza kuwa, wananchi wote waliopisha mradi huo kwenye eneo la kiwanda lenye ekari 98.7 wameshalipwa fidia.
Awali Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi alisema kuwa mradi huo una manufaa mengi kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ikiwemo kupata ajira kwenye kazi zinazoendelea sasa, Kijiji cha Sojo kupata umeme wa gridi ndani ya wiki moja ijayo na pia kijiji kitafaidika na ujenzi wa kituo cha afya.
Akiwa mkoani Tabora, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba pia alikagua kazi za usambazaji umeme pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wilayani Igunga katika kitongoji cha Mwabula ambapo kunafanyika shughuli za uchimbaji madini na kuahidi kuwa vijiji vyote wilayani humo vitapata umeme.
Pia, aliwaeleza wachimbaji wadogo katika eneo hilo kuwa, migodi yao itasambaziwa umeme kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wilaya ya Igunga ina maeneo Sita ya Wachimbaji wadogo yatakayofaidika kwa kuanzia huku Mkoa wa Tabora kwa ujumla ukiwa na maeneo 10 ya wachimbaji wadogo yatakayosambaziwa umeme na REA.
Vilevile, Waziri wa Nishati alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Ugaka wilayani Igunga na kupata wasaa wa kuzungumza na Bw. Kasindi Joseph ambaye ni mmoja wa wananchi aliyetumia fursa ya umeme kufika kijijini hapo kwa kufungua mashine ya kukoboa na kusaga nafaka pamoja na mashine ya kukamua alizeti.
Bw. Joseph alimweleza Waziri kuwa, anahitaji umeme wa kutosha ili kufanya shughuli zake kwa ufanisi ambapo Waziri wa Nishati, aliwaelekeza watendaji wa TANESCO kufunga transfoma itakayokuwa na uwezo wa kutoa umeme wa kutosha kwenye kijiji hicho ili kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi.
Akiwa kijijini Ugaka, Waziri wa Nishati pia alipata wasaa wa kuzungumza na Bw. Shaban Ali ambaye kwa sasa anafanya biashara ya mafuta kwa njia ya chupa na madumu, hata hivyo, mwananchi huyo amekuwa ni mnufaika wa kwanza atakayepata fedha za mkopo zilizotengwa na Serikali kupitia REA ili kuwawezesha wajasiriliamali kufungua vituo vidogo vya mafuta vijijini ili kuuza mafuta safi, kwa njia salama na kwa bei elekezi.