Na Alfred Mgweno (TEMESA)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kujenga kivuko kipya kitakachokuwa na uwezo wa kubeba abiria 3000 na magari 80 kwa wakati mmoja kwa wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam kutokana na uhitaji mkubwa wa usafiri unaowakabili wakazi wa maeneo hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko cha MV. KAZI unaoendelea katika Yadi ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kauli ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ni muendelezo wa ahadi aliyoitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Desemba 6, 2021 wakati aliposimama kuzungumza na wananchi wa Kibada Kigamboni alipokuwa akielekea kwenye uzinduzi wa kiwanda kilichopo Kisarawe 11, Kigamboni ambapo Mhe. Rais aliahidi kuleta Kivuko kingine kipya kwa wananchi wa Kigamboni kutokana na adha ya usafiri wa maji wanayokumbana nayo katika eneo hilo.
“Suala la uchakavu wa vivuko vinavyovusha watu Kigamboni, niwaambie kuwa hili lipo ndani ya mipango yetu tunalifanyia kazi tuone uwezekano wa kupata kivuko kikubwa chenye kuchukua watu wengi na mizigo mingi ili kupunguza safari za vivuko vidogo kwenda na kurudi,” alisema Rais Samia Desemba 6, 2021.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kukagua ukarabati wa kivuko hicho, Profesa Mbarawa amesema mji wa Kigamboni na viunga vyake unakua kwa kiasi kikubwa sana hivyo kutokana na kuongezeka kwa wakazi maeneo hayo, Serikali imeamua kuwa itajenga kivuko kipya kitakachokuwa kinatoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni ili kupunguza kero ya usafiri kutokana na uwepo wa abiria wengi wanaotumia huduma za kivuko.
''Tumeamua kujenga kivuko kipya ambacho kitachukua watu 3000 kwa mpigo na magari 80, MV.KAZI inachukua watu 800, MV.MAGOGONI inachukua watu 2000, lakini kivuko kitakachokuja kitachukua watu elfu tatu kwa mpigo. tunaamini vivuko vyote hivi kwa pamoja kama vitafanya kazi vizuri naamini tatizo la usafiri katika maeneo kati ya Magogoni na huku Kigamboni utaisha kabisa''. Alisema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba baada ya bajeti kuanza ya mwaka 2022/2023 zitatengwa fedha kwa ajili ya kuanza mara moja kwa ujenzi wa kivuko hicho kipya.