Na. Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Ujenzi wa Mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Ifakara kilichoanza kujengwa mwezi Machi, 2020 kinatarajiwa kuhudumia Wananchi takriban 100,000 wa wilaya za Kilombero na Ulanga.
Hayo yamezungumzwa leo katika mji wa Ifakara, wilayani Kilombero mkoani Morogoro wakati Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na Wanahabari kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo hicho na Kilomita 82 za miundombinu ya usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.
Mhandisi Saidy amesema kuwa, ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 80.1 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2023 ambapo mpaka sasa tayari transifoma ya kisasa imeshawekwa na kituo kitatoa njia nne za umeme ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali.
Akizungumza kuhusu kurefusha njia za kusambaza umeme, amesema kuwa mradi huo umeshakamilika na njia hizo zenye jumla ya kilomita 82 zitaweza kufikia vijiji na vitongoji takribani 15 katika wilaya ya Kilombero.
"Kwa muda mrefu Wananchi wa maeneo haya walikuwa wanapata changamoto ya kukatika kwa umeme na kupungua kwa nguvu ya umeme inayopelekea kuunguza vifaa na hata mitambo, hivyo mradi huu utaondoa adha ya umeme kukatika na utaboresha ubora wa huduma," alisema Mhandisi Saidy.
Mradi huo wa kituo cha kupoza umeme na kilomita 82 za miundombinu ya usambazaji wa umeme vinagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Ulaya kwa gharama ya EURO milioni 8.75 ambapo Kituo cha kupoza umeme pekee kimegharimu EURO milioni 5.4.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, Rodney Thadeus amesema kuwa nishati inafungamanisha na maendeleo mengine ya kiuchumi ambapo Serikali imeendelea kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo hospitali na shule pamoja na kuwawezesha Wakulima, hivyo ukosefu wa nishati utafanya shughuli hizo kutokwenda vizuri.
"Natoa rai kwa Wananchi kushirikiana na Serikali katika kuibadilisha Tanzania kupitia REA ambayo inaendelea kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha wanapata nishati", alisema Bwana Thadeus.