Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kikao Uimarishaji Mpaka Tanzania na Kenya Chaanza Tarime
Apr 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM TARIME

Kikao cha Kamati ya pamoja ya Wataalamu wa mipaka kati ya Tanzania na Kenya kimeanza leo tarehe 11 Aprili, 2022 wilayani Tarime mkoani Mara.

Kikao hicho cha Kamati ya Pamoja kati ya nchi hizo mbili kinachotarajiwa kumalizika Aprili 15, 2022 wilayani humo, kitapokea mawasilisho ya kazi iliyofanyika na kutoa muongozo juu ya namna bora ya kutekeleza kazi iliyobaki. 

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho wilayani Tarime mkoani Mara kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mangwela alisema uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Kenya ulenge kuimarisha mahusiano ya nchi hizo pamoja na kujadili changamoto za maeneo ya mipakani.

"Pamoja na kuimarishwa mipaka kati ya Tanzania na Kenya lakini bado kuna maeneo ambayo baadhi ya wananchi kutoka kila upande wanaingia na kuendesha shughuli zao hivyo mjadili changamoto hizi kwa kina na kuja na maamuzi yatakayoleta tija", alisema Kanali Mangwela.

Timu ya wataalamu wa Tanzania na Kenya imefanikiwa kukamilisha uimarishaji mpaka wa kimataifa wa awamu ya kwanza na kuanza awamu ya pili iliyosimama kutokana na changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Balozi Joseph Vungo aliwataka wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kuhakikisha wanajadili na kuzitolea maamuzi changamoto kwa amani hasa wakizingatia nchi ya Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri.

Kwa mujibu wa Balozi Vungo, maamuzi yoyote yatakayoamuliwa katika kikao hicho yalenge kuleta tija na kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo.

Zoezi la uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya awamu ya kwanza limeanzia katika Hifadhi ya Serengeti / Masai Mara kipande cha Kilomita 60 hadi  eneo la Ziwa Natron kilomita 23 na awamu ya pili inaanzia Ziwa Natron hadi Namanga eneo la Kilomita 110.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi