Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kikao Kazi Kati ya Serikali na NGOs Nchini
Jan 26, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu,

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekutana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kikao kazi cha kuweka mwelekeo wa Ushirikiano miongoni mwao na kutafuta ufumbuzi wa changamoto katika kufikia maendeleo yanayokusudiwa.

Kikao hicho cha kihisitoria, kimefanyika Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao hicho alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 350 kutoka Serikalini na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu, Dkt. John Jingu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo nchini.

Aidha, amesema Serikali kwa nyakati tofauti imeanzisha na kusimamia Sera, Kanuni na Miongozo mbalimbali ili kuwezesha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji shughuli za Serikali na Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

 “Ukiniuliza sasa hivi, naweza kukueleza mchango wa NGOs katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kupitia sekta mbalimbali iwe katika sekta za maji, elimu, afya ardhi na nyinginezo nyingi” Alisema Dkt. Jingu.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga amewataka wadau wa NGOs kutumia kikao kazi hicho kama fursa ya kupata muelekeo wa kuboresha mapungufu na kutatua changamoto zilizopo katika Sekta ya NGOs.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS), Francis Kiwanga ameeleza kufurahishwa na hatua ya Serikali kukutana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuwa hiyo ndicho chanzo cha mazungumzo kati ya pande hizo mbili na Mkutano wa Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali  ni hatua muhimu na chanzo cha kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga amesema Kikao cha aina hiyo kitaepusha malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza hapo awali ambapo sasa wadau wamepata fursa ya kuzungumza changamoto zao.

Ameongeza kwa kupongeza Serikali kwa kushiriki mazungumzo na Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali ni lango la kuingia katika meza ya mazungumzo na kuainisha changamoto na kutafuta ufumbuzi wake.

Kikao Kazi cha Siku mbili kati ya Serikali na NGOs , kinalenga kuboresha uhusiano kati ya pande hizo mbili, kutambulisha mchango wa NGOs katika maendeleo ya Nchi, pamoja na Uratibu na Usimamizi wa Mashirika hayo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi