Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kigamboni Yachapa Mwendo Uwekaji Anwani za Makazi
Apr 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Abubakari Kafumba, Kigamboni – Dar es Salaam

Wilaya ya Kigamboni imeendelea kuchapa mwendo katika uwekaji wa Anwani za Makazi huku zoezi zima likiwa limefikia asilimia 84.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, James Mkumbo ameeleza kuwa Kigamboni ambayo ina Tarafa tatu za Somangila, Pemba Mnazi na Kigamboni, Kata 9, Mitaa 67 na wakazi wapatao 238,591 imeendelea na zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi kwa ufanisi mkubwa ambapo mpaka sasa kata 6 kati ya kata 9 zimefikiwa.

 “Eneo kubwa la Manispaa ya Kigamboni ambalo ni 70% ya eneo zima limepimwa hivyo imeongeza ufanisi mkubwa wa utekelezaji wa zoezi hili hasa katika hatua ya kuzitambua nyumba na eneo zilipo, wapi zoezi linapaswa kusogezwa na kutambua maeneo ambayo hayajaendelezwa ili kuchochea maendeleo katika maeneo hayo.

Kwa kutumia kikosi kazi maalum cha wataalamu 11 wa kusoma ramani, maeneo yote yametambulika na taarifa zimeendelea kuchukuliwa bila kuacha mtu nyuma”, ameeleza Bw. Mkumbo.

Amesema kuwa hadi sasa kaya 41,540 zimefikiwa katika uwekaji wa namba za nyumba sawa na asilimia 84 ya zoezi zima ambapo mkakati uliopo ni kukusanya taarifa takriban nyumba 3,000 kwa siku huku lengo kuu likiwa ni kuzifikia kaya 49,353 kwa ujumla.

“Uwekaji wa taarifa hizo za wakazi kwenye kanzidata unaendelea na umefikia asilimia 26 na kwamba zoezi hilo linaendelea kuboreshwa ili kuwafikia wakazi wote wa Kigamboni na hatimaye zoezi hilo kukamilika kwa 100% ifikapo Mei 2022”, amesisitiza Mkumbo.

Ameeleza kuwa katika Wilaya ya Kigamboni, zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi ambalo pia linaendelea nchi nzima limekuwa na faida nyingi za kijamii kwa Wana-Kigamboni ikiwemo fursa za ajira katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za kuiendeshaji kama vile wataalamu wa TEHAMA, wakusanyaji taarifa, wahifadhi taarifa kwenye kanzidata, waweka namba za nyumba 140, wasoma ramani 11, mafundi vyuma wanaotengeneza vibao na wataalamu wengine wanaochangia kufanikisha mchakato mzima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi