Na. Lilian Lundo - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuingia madarakani alitangaza kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya sita kuwa ni “Kazi Iendelee” akiwa na maana ya kuyaendeleza mazuri ya awamu zilizopita.
“Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopita na kuleta mema mengine mapya na hii kimsingi ndiyo salamu yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee” alifafanua Rais Samia alipokuwa akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021.
Rais Samia alisisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza mipango na dira ya maendeleo ambayo iliandaliwa na utawala uliopita kwa kuzingatia ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika kipindi cha mwaka mmoja madarakani, Rais Samia ametekeleza kauli mbiu hiyo ya Kazi Iendelee kwa vitendo ambapo tumeona miradi mbalimbali iliyoachwa na Hayati John Pombe Magufuli ikiendelezwa kwa kasi na Serikali ya Awamu ya Sita.
Profesa Humphrey Moshi, Mchumi Mbobezi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, anaeleza namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyofanikiwa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yake ya ‘Kazi Iendelee ambapo alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya, licha ya changamoto ya ugonjwa wa UVIKO unaotikisa Dunia nzima, lakini bado tunaona miradi mbalimbali iliyoachwa na Hayati Magufuli ikiendelezwa na Rais Samia.
“Kazi Iendelee ina mashiko, kwa sasa tunaona Rais Samia anatekeleza kwa vitendo miradi yote ya awamu ya Tano, mfano ukamilishaji wa daraja jipya la Selander, uendelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, uendelezaji wa mradi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi Mbagala na miradi memngine mingi,” alifafanua Prof. Moshi.
Aliendelea kusema kuwa, licha ya kuendeleza miradi ya awamu zilizopita, , kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona shilingi Tril. 1.3 imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ununuzi magari, ujenzi wa vituo vya dharura na vifaa kwa hospitali, utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi.
Prof. Moshi aliendelea kusema kuwa, kasi ya kuhamasisha utalii inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ni jambo muhimu kwa uchumi wa nchi, kwani italeta ukombozi wa uchumi.
“Sekta ya utalii ndio ukombozi wa uchumi, tuna Hifadhi zaidi ya 22 nchini, kama zikitangazwa vizuri zitaleta watalii, ambapo wanapokuja kwa wingi wanaacha fedha za kigeni ambazo zinasaidi kuimarisha fedha zetu za ndani,” alifafanua Prof. Moshi.
Aidha ameeleza, suala la nchi kuchukua mikopo, ni suala ambalo haliepukiki kama tunataka maendeleo. Aidha amesema kuwa, hata kwa mtu binafsi huwezi kuendelea kama hukopi, na unaposema huchukui mikopo ni sawa na kusema hutaki kuona benki zikiendelea, kwani benki zinaendeshwa kwa mikopo inayoitoa.
Prof. Moshi amewataka Watanzania kumuunga mkono na kumpa ushirikiano Rais Samia, kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kama ni mfanyabiashara kwa kulipa kodi kama inavyotakiwa vilevile kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na umma, pia vijana wawe na nidhamu na kufanya kazi kwa bidii.
“Tukimpa ushirikiano Rais wetu tutakuwa na amani, na nguzo kubwa ya kukua kwa uchumi wa nchi ni uwepo wa amani katika nchi. Amani inapokesekana nchi inakuwa haipo katika utulivu, hivyo kusababisha mambo mengi kutoendelea ipasavyo,” alifafanua Prof. Moshi.