Takribani kaya 525 zimejindikisha tayari kuhama kwa hiari kutoka katika eneo la Ngorongoro kwenda eneo la Msomera na maeneo mengine katika awamu ya pili ya mpango wa wananchi kuhama kwa hiari.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea maeneo ya Ngorongoro na msomera kujionea hali halisi ya zoezi la wananchi kuhama kwa hiari.
“Katika zoezi la kuhama awamu ya kwanza ilifanyika, sasa tupo katika awamu ya pili, hii awamu ya pili kufikia Januari 12, 2024 kulikuwa na kaya 525 ambazo zimejiandikisha na zikiwa tayari kuhama kutoka Ngorongoro.
Aidha, ameeleza kuwa, kila kaya ikijiandikisha inafanyiwa tathimini ya mali, hivyo baada ya hayo mwananchi analipwa fidia ya mali zake,kusafirishiwa mizigo, kupewa shilingi milioni 10 na nyumba ya vyumba vitatu iwapo anakwenda eneo la Msomera, Sauni, Kitwai na shilingi milioni 15 kwa maeneo mengine atakayochagua kwenda.
“ Mwananchi yule anasafirishwa yeye na familia yake na mifugo yake kwenda katika eneo ambalo amelichagua na kama ni hapa Msomera akifika anapewa chakula cha miezi 18 ambayo ni magunia mawili ya mahindi kwa kila miezi mitatu” ameongeza Bw. Matinyi.
Kadhalika, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa, kati ya kaya ambazo zimejiandikisha na kutaka kuhama kwa hiari kuna jumla ya kaya 126 zimeshahama ambapo kaya hizo zina watu 812 na zinamifugo 2581 na zimegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza limekwenda Msomera lina kaya 74 zenye watu 520 na mifugo 1599 na kundi la pili wamechagua mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Manyara, Simiyu, Tanga Pwani na maeneo mengine ambazo ni kaya 52 zenye watu 292 na mifugo 982.
Mbali na hayo, kuhama kwa wananchi kutoka Ngorongoro kwenda Msomera kutasaidia eneo la Ngorongoro kuondoa tatizo la mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa mazingira na kuota kwa mimea isiyo rafiki kwa wanyama pamoja na kuondoa tatizo la magonjwa ya wanyamapori kuingiliana na mifugo.
Zoezi la uhamaji kwa hiari linaendelea ambapo Januari 18, 2024, kutakuwa na kundi lingine la kaya 72 lenye watu 515 ambalo litaondoka Ngorongoro, hata hivyo mpaka sasa kaya 677 zimeshahama kwa hiari kutoka Ngorongoro zikiwa na watu 3,822 na mifugo 18,102.