Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kaya 3000 kusambaziwa Gesi Dar
Oct 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_20488" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiwa na Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Engie, Johan Kerrebroeck katika Ofisi ya Waziri jijini Dar es Salaam.[/caption]

Na.Teresia Mhagama -DSM

Waziri wa Nishati,  Dkt Medard Kalemani ameeleza kuwa jumla ya kaya 3000 zitasambaziwa nishati ya Gesi katika Jiji la Dar es Salaam ndani ya miaka miwili au zaidi mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa usambazaji gesi mwezi Aprili mwaka 2018.

Dkt.Kalemani aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa  kampuni ya Engie ya Ufaransa, Johan Kerrebroeck ambaye alifika wizarani ili kueleza nia ya kampuni yake katika kuwekeza kwenye mradi huo pamoja na miradi mingine ya uzalishaji Umeme kwa kutumia Gesi Asilia ukiwemo wa Somanga Fungu wa megawati 240.

Waziri huyo wa Nishati alisema kuwa mradi huo wa usambazaji Gesi  utaelekezwa  pia katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo kaya zaidi ya 1500 zinatarajiwa kufaidika.

[caption id="attachment_20491" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akimsikiliza Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Engie, Johan Kerrebroeck (wa pili kushoto) katika Ofisi ya Waziri jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Nishati-Maendeleo ya Nishati, James Andilile (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Haji Janabi (wa pili kulia) na Mhandisi Msafiri Baraza kutoka Wizara ya Nishati.[/caption]

“ Hatutaishia katika mikoa hiyo tu bali baada ya hapo tutasambaza katika mikoa mingine nchini kama Morogoro, Dodoma na Pwani  na katika magari,” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, usambazaji wa Gesi majumbani utasaidia kutunza mazingira kwani utapunguza matumizi ya Mkaa ambayo ni zaidi ya asilimia 90 nchini, jambo ambalo linachangia sana katika uharibifu wa mazingira.

Waziri wa Nishati, aliikaribisha kampuni ya Engie  kuwekeza katika usambazaji wa Gesi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kuhusu suala la kuwekeza katika mradi wa uzalishaji Umeme wa megawati 240 kwa kutumia Gesi Asilia wa  Somanga Fungu, Dkt Kalemani alisema kuwa upembuzi yakinifu wa mradi huo utakamilika mwezi Aprili mwaka 2018 hivyo baada ya hapo ndipo hatua nyingine za uendelezaji mradi zitakapoanza kufanyika kwa kukaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

[caption id="attachment_20494" align="aligncenter" width="750"] Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Engie, Johan Kerrebroeck (wa kwanza kulia) akisalimiana na Mhandisi Nishati Mkuu, Salum Inegeja katika Ofisi ya Waziri wa Nishati jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kamishna Msaidizi wa Nishati-Maendeleo ya Nishati, James Andilile.[/caption]

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa  kampuni ya Engie, Johan Kerrebroeck alitumia fursa hiyo kumpongeza Dkt. Kalemani kwa kuteuliwa kuwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati nchini.

Aidha alisema kuwa kampuni yake ina uzoefu wa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya Nishati katika nchi mbalimbali duniani  ikiwemo Peru na Mexico. Nchini Tanzania, kampuni hiyo imewekeza katika mradi mdogo wa Umeme Jua wa Kilowati 16 katika Kijiji cha Ketumbeine mkoani Arusha.

Kampuni ya kimataifa ya Engie imejikita katika uendelezaji wa miradi ya  Umeme, Gesi Asilia na huduma nyingine za Nishati  ambapo inafanya shughuli zake katika nchi  70 duniani.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi