Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha Amour, amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma na kiwanja cha ndege cha Msalato kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Akizungumza mara baada ya kagua utekelezaji wa miradi hiyo jijini hapo, Balozi Aisha amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha miradi hiyo kudumu kwa muda mrefu na kuweza kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
"Sisi kama Serikali tunataka kuona ubora wa kazi, miradi hii ikikamilika vizuri na kwa ubora itarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani na hivyo kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla", amesema Balozi Aisha.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amewataka makandarasi hao kuhakikisha kuwa wanatatua mapema changamoto zote zinazowakabili ili kuhakikisha miradi hiyo haikwami na inakamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mkataba.
Ameusisitiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo, kukagua na kufuatililia kwa karibu hatua kwa hatua utekelezaji wa miradi hiyo ili kuona kuwa thamani ya fedha inayotumika inaendana na mkataba.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda, amesema kuwa kwa sasa ujenzi wa mradi huu sehemu ya kwanza ya Nala- Veyula- Mtumba- Ihumwa Bandari Kavu ( Km 52.3) umefikia asilimia 8.5 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2024.
Kwa upande wa Kiwanja cha ndege cha Msalato, Mhandisi Kabunda amesema kuwa hadi sasa Mkandarasi amekwishamaliza ujenzi wa kambi yake ya kuishi, karakana, bohari pamoja na mtambo wa kuzalisha kokoto na tofali.
Ameongeza kuwa ujenzi wa Kiwanja hiki unatarajiwa kujengwa kwa sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza itahusisha ujenzi wa miundombinu ambayo itajumuisha sehemu ya kurukia ndege, sehemu ya kupaki, njia ya ndege, maegesho ya magari, uzio, mageti pamoja na barabara za maingilio.
Mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato unajengwa na Mkandarasi Sinohydro Corporation Limited kwa kushirikiana na M/s Beijing Sino - Aero Construction Engineering Co. Ltd na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2025.