Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Katibu Mkuu Maliasili Afungua Mkutano wa Kamati Tendaji Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu
Jun 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka amefungua mkutano wa tatu wa Kamati Tendaji ya Mradi Jumuishi wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Wanyamapori Tanzania.

Mradi huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo Juni 27, 2022 uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma, Prof. Sedoyeka amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi na kutoa mwongozo kwa Kitengo cha Usimamizi wa Mradi ili kifanye kazi kikamilifu kufikia lengo la Serikali la kutokomeza ujangili ifikapo mwaka 2025.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inasimamia ushirikiano kati ya washirika na wadau katika utekelezaji wa mradi huo ili kufikia dira ya Sera ya Taifa ya Wanyamapori inayolenga kulinda wanyamapori na makazi yao, usimamizi namaendeleo ya rasilimali za wanyamapori na kuzuia matumizi haramu ya wanyamapori.

Aidha, Prof. Sedoyeka amesema kuwa mradi huo ulilenga pamoja na mambo mengine, kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili na Mkakati wa Usimamizi wa Maeneo ya Wanyamapori, kupitia kanuni za uwindaji wa Kitalii, kuwajengea uwezo watumishi katika kupambana na ujangili, kuwezesha wananchi katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu na kuboresha maisha yao kwa kushiriki katika usimamizi wa wanyamapori.

Pia amefafanua kuwa mradi umefanikiwa kununua Land cruiser Hard top kumi (10) mpya ili kusaidia utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori. 

Mkutano huo umehudhuriwa na Amon Manyama kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo Duniani (UNDP), Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji wa Mradi na Kitengo cha Usimamizi wa Mradi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi