Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Katibu Mkuu Maganga Atoa Wito Kupunguza Uchomaji Holela wa Taka
Nov 22, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga amezitaka nchi zinazotekeleza Mradi wa Kupunguza Uzalishaji wa Kemikali Sumu aina ya uPOPs zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu zinazotokana na uchomaji holela wa taka kuchukua hatua za kupunguza uchomaji holela wa taka hizo ili kuhifadhi mazingira.

Ametoa wito huo juzi jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinazotekeleza mradi huo.

Bi. Maganga alizitaka nchi hizo kuhakikisha zinafikia malengo yaliyowekwa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuhuisha taarifa muhimu za kikanda zinazohusu uchomaji holela wa taka kwa kuwa na kanzidata.

Pia alisema wananchi wa mataifa wanufaika wa mradi wanapaswa kuelimishwa kuhusu madhara yatokanayo na uchomaji holela wa taka na hatua zinazochukuliwa na kila nchi katika kukabiliana na athari zitokanazo na uchomaji holela wa taka.

“Malengo ya mafunzo katika warsha hii ni kukuza uelewa na ujuzi kwa washiriki kuhusu kupunguza na kudhibiti uchomaji holela wa taka, hatua za kutatua changamoto za usimamizi wa kemikali nchini pamoja na kuweka malengo ya pamoja ya kupunguza uzalishaji wa kemikali aina ya uPOPs,” alisisitiza.

Warsha hiyo inahusisha washiriki kutoka nchi saba wanachama wa SADC zinazotekeleza mradi huo ambazo ni Botswana, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Msumbiji, Tanzania na Zambia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi