Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Katibu Mkuu Katiba na Sheria Awataka Polisi, Magereza Kuhakikisha Haki za Mtoto Zinalindwa
Jul 22, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na. Karimu Meshack, Mbeya

Serikali imewataka Polisi na Magereza nchini kuhakikisha haki na maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika Mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.

Prof. Mchome amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wakiwemo UNICEF na wengine, imeendelea kuzingatia maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.

“Ni rai yangu kuwa mnapokabiliana na kesi za watoto hakikisheni mtoto anapata msaada wa kisheria mara unapokutana naye au kusikia habari zake. Kwa kuwa mtakutana na watoto wa namna hii, ninaomba mafunzo haya yawakumbushe wajibu wenu katika kumhudumia mtoto ili haki itendeke kwa wakati.”

Hivi karibuni, Mhe. Jaji Mkuu alitoa Kanuni za ushughulikiaji wa mashauri yanayohusu watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo watoto. kanuni hizo zinaweka masharti ya kuhakikisha upelelezi, uendeshaji na utoaji wa hukumu kwa mashauri ya watoto unafanyika kwa wakati kutokana na changamoto zilizopo katika mashauri hayo amesisitiza Prof. Mchome.

Aidha, Prof. Sifuni Mchome ametaja hatua za zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mfumo wa haki jinai kuwa ni marekebisho ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kwa kuweka utaratibu wa kufifisha makosa na kuimarisha mfumo wa upatanishi katika makosa ya jinai kwa lengo la kupunguza mrundikano wa mashauri Mahakamani na kuondoa msongamano wa mahabusu na wafungwa katika vituo vya polisi na magereza, hivyo kuwataka mafisa wa polisi na Magereza kuzitumia njia hizo.

“Ninyi mnaopatiwa mafunzo haya mnapaswa kuwa mabalozi kuonesha mfano kwa kuzitumia njia hizi kwani zipo kwa mujibu wa sheria kuwezesha mfumo huo kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria. Kutokana na Wizara yangu kusimamia masuala ya utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria na mfumo wa haki jinai, ni imani yetu kuwa, kama wadau wakubwa, mtaitumia fursa hii kujitathimini na kushiriki kujenga mfumo wa utoaji haki wenye tija usio na malalamiko kwa wananchi”, alisema.

Akiwashukuru UNICEF kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuhifadhiwa Prof. Mchome amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto zinazomkabili mtoto anayekinzana na sheria katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na UNICEF pamoja na wadau wa haki mtoto,  imeandaa Mkakati wa Haki Mtoto ambao hivi karibuni utazinduliwa. Mkakati huu unalenga kuhakikisha kuwa wadau wa masuala ya mtoto wanafanya kazi kwa pamoja katika kusimamia masuala ya haki mtoto.

“Moja ya wadau wakubwa katika mkakati huu ni Jeshi la Polisi na Magereza ambapo jukumu lenu ni kubwa mno katika masuala ya haki mtoto. Mkakati huu unawalenga watoto wote walioathirika na ukatili wa kijinsia, waliotenda makosa au kujikuta kizuizini kutokana na mzazi kutenda kosa.”

Ni wazi kwamba Mkakati huu kitakuwa chombo kinachoaminika na sehemu salama kwa mtoto tofauti na ilivyo sasa ambapo kumekuwa na malalamiko ya watoto kupewa umri mkubwa tofauti na uhalisia, amesisitiza Prof. Mchome.

“Ni rai yangu kwamba Wadau wote tutashirikiana katika kuhakikisha ulinzi na ustawi wa mtoto linakuwa ni jukumu letu la msingi. Hivyo, nawahimiza kwa mara nyingine kujaribu kutumia njia mbadala za kushughulikia masuala yanayohusu haki za mtoto badala ya kujielekeza katika kuwaweka vituoni au magereza jambo linalosababisha msongamano.

"Mwaka 2017 Wizara ya Katiba na Sheria ilisimamia mchakato wa kutunga na kupatikana kwa sheria ya Msaada wa Kisheria Na 1 ya 2017. pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo ina lengo la kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili.

Aidha, sheria hii imeweka masharti ya kutoa msaada wa kisheria katika mashauri ya jinai. Ni kwa muktadha huo, Wizara ya Katiba na Sheria iliingia makubaliano na Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2018 kuhusu utekelezaji wa masuala ya msaada wa kisheria katika vituo vya Polisi na magereza nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi