Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kasekenya Atoa Mwezi Mmoja kwa TBA Kukamilisha Nyumba ya Jaji wa Shinyanga
Dec 14, 2022
Kasekenya Atoa Mwezi Mmoja kwa TBA Kukamilisha Nyumba ya Jaji wa Shinyanga
Muonekano wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga linalojengwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 mkoani humo.
Na MAELEZO

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametoa mwezi mmoja kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa jengo la Mhe. Jaji Kanda ya Shinyanga ili aweze kuhamia na kutumia jengo hilo.

Amezungumza hayo mkoani Shinyanga mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo pamoja na jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu linalojengwa na Vikosi  vya Ujenzi na kusimamiwa na Wakala huo ambapo amesisitiza Wakala huo kujenga majengo bora yatakayodumu kwa kipindi kirefu.

 Muonekano wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu linalojengwa na Vikosi vya Ujenzi na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 65 mkoani Shinyanga. 

“Hakikisheni mnamsimamia Mkandarasi ili ajenge kwa viwango hivyo hivyo vilivyopo katika usanifu”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Awali akitoa taarifa ya miradi hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Nestory Nanguka, ameeleza kuwa mpaka sasa utekelezaji wa jengo la Mhe. Jaji Kanda ya Shinyanga umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu umefikia asilimia 65.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ambapo atakagua miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Nestory Nanguka (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) wakati akikagua ujenzi wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga linalojengwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 mkoani humo. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amekagua Daraja la Negezi (m 60) katika barabara ya Kanawa – Mihama lililojengwa na kukamilika mwaka huu kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.8.

Amesema Serikali iliamua kujenga daraja hilo kubwa kutokana na uwepo wa daraja dogo lililojengwa toka mwaka 1954 ya njia moja ambalo halikukidhi mahitaji ya wananchi na kusababisha adha kubwa hasa kipindi cha masika.

Kasekenya amewataka wananchi hao kulitunza Daraja hilo kwa kutofanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa daraja.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ambapo atakagua miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi