Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema Kampuni ya madini ya Acacia imekuabali kufanya mazungumzo na Serikali ikiwa ni pamoja na kulipa fedha ambazo Serikali inadai kwa kufanya shughuli zake hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation inayomiliki kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton leo Ikulu jijini Dar es Salaama, Rais Magufuli amesema kampuni ya Barrick imekubali mazungumzo na Serikali ya Tanzania na kulipa fedha wanazodaiwa.
“Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ilikufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alisema kuwa licha ya kampuni hiyo kukubali kulipa fedha wanazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu hapa nchini.
Naye, Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili ikiwa ni pamoja na kulipa fedha zote ambazo inatakiwa kulipa kwa Serikali ya Tanzania.
Mazungumzo hayo kati ya Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Acacia yalihudhuriwa na Balozi wa Canada nchini Ian Myles naWaziri wa Katiba na sheria Prof. Palamagamba Kabudi.