Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Uchunguzi ya Bwawa la Matope Mgodi wa Mwadui Yakabidhi Ripoti
Nov 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Michael Utouh - Shinyanga


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema amepokea ripoti ya uchunguzi wa bwawa la matope lililovunja kuta na kuelekea katika makazi ya wananchi mnamo tarehe 07.11.2022 katika mgodi wa Williamson Diamond limited uliopo Mwadui katika wilaya ya Kishapu.


Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph  Mkude amesema anamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwa alikuwa ni wa kwanza baada ya kuripotiwa kwa janga hilo lililotokea katika mgodi aliweza kufika na kwa haraka na kuunda Tume itakayochunguza chanzo cha hadi kubomoka kwa bwawa.


Amesema kuwa lengo la kamati hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha kubomoka kwa bwawa, kubaini madhara yaliyotokea, kubaini madhara ya maji tope, lakini pia lengo lingine ni kutoa ushauri na mapendekezo ya nini kifanyike na kufahamu hatua zilizochukuliwa na Serikali, Mgodi pamoja na kuangalia kama kuna madhara yaliyojitokeza baada ya kubomoka kwa bwawa hilo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema amesema anaishukuru kamati hiyo ya uchunguzi ambayo imefanya kazi yake kwa weledi mkubwa na ufanisi hadi siku ya leo wanapoikabidhi kwake baada ya kufanya kazi ya uchunguzi kwa muda wote wa siku 14 toka alipoikabidhi kamati hiyo jukumu hilo.


Amesema ripoti hiyo ataifikisha kwa Waziri husika wa Madini, Mhe. Doto Biteko  na kupelekwa Baraza la usalama la mazingira ( NEMC) ambao ndio watakaotoa maamuzi ya mwisho baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.


Aidha, Mhe. Mjema ameongeza kwa kusema Kamati hiyo aliyoiunda iliunganisha wataalamu wote wanaohusika katika kutoa taarifa iliyo kamili baada ya kubomoka kwa bwawa hilo na sivyo kama wengi walivyokuwa wakidhani kamati aliyoiunda ni ya ulinzi na usalama tu.

  Ametaja waliohusika katika kuandaa ripoti hiyo kuwa ni pamoja na wataalamu kutoka NEMC, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, wataalamu kutoka Bonde la maji kati, wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kamati ya usalama ya Mkoa pamoja na ofisi ya DED Kishapu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi