Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Mhe. Hamisi Shomari ameingoza kamati hiyo kutembelea miradi miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 9 inayotekelezwa kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.
Ziara hiyo imefanyika leo Jumatatu Oktoba 30,2023, ambapo wamatembelea barabara ya Picha ya Ndege-Sofu inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) yenye thamani ya shilingi 943,600,000/- ikiwa na urefu wa mita 700 na kuhitimisha ziara Soko la Kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni 8 linalomilikiwa na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Mhe. Shomari ameridhika na hatua ya ujenzi kwenye miradi yote na kutoa rai kwa TARURA kumaliza kwa wakati kipande kingine chenye urefu wa mita 700 kwa gharama ya shilingi 943,600,000/- ili kutoa fursa kwa wananchi kutembea kwenye lami inayogharamiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiwa ni utekelezaji wa IIani ya Uchaguzi ya 2020-2025
Diwani wa Kata ya Viziwaziwa, Mhe. Masoud Mohamedi Chamba ameiomba Serikali kuendelea kuikumbuka Wilaya ya Kibaha kwenye mtandao wa Lami kupitia mradi wa TACTIC kwani bado ipo nyuma ukilinganisha na maeneo mengine yenye hadhi ya Makao Makuu ya Mkoa.
Akizungumzia Soko la Kisasa, Mhandisi Brighton Kisheo amesema ujenzi umefikia asilimia 99 na kwamba Mkandarasi kwa sasa anamalizia sehemu ndogondogo na kwamba muda wowote litaanza kupangishwa kwa wawekezaji kufanya biashara.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mhe. Mussa Ndomba amesema Waheshimiwa Madiwani wataendelea kusimamia miradi yote ndani ya halmashauri ili thamani ya fedha ilingane na miradi inayotekelezwa na kuwanufaisha wananchi.