Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Yaridhishwa na Mradi wa Timiza Malengo
Sep 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu – Morogoro

Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu , Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo unaotekelezwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.

Hayo yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Alice Kaijage wakati wa ziara ya Kamati ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa  mradi huo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro  ambapo alisema kuanzishwa kwa mradi kumewafanya vijana kuamka kifikra na kuamini  wana uwezo wa kujieletea maendeleo.

Mradi huo unatekelezwa ikiwa ni Awamu ya Pili kuanzia mwaka  2021 hadi  mwaka 2023 katika Halmashauri  za Wilaya 18 zilizopo katika   Mikoa mitano  ya Dodoma, Geita, Morogoro, Singida na Tanga ukihusisha vijana wanaotoka katika Kaya masikini.

“Katika Halmashauri ya Ifakara tumekuta Serikali na watendaji wanafanya kazi kwa bidii sana tumewaona vijana wana ujasiri, wamefungua miradi, biashara, wengine wanafuga kuku, nguruwe na kufungua magenge ni kwa sababu Serikali kupitia watendaji imewawezesha vijana hawa na imewasaidia kuepuka vishawishi mbalimbali,” Alisema Dkt. Alice.

Pia aliwataka vijana hao kusimamia malengo yao kwa kutumia vyema fedha walizopewa ili kuainisha miradi hatua itakayosaidia kuepuka vishawishi vitakavyosababisha kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutokana na hali duni ya maisha.

“Afua mojawapo katika kutekeleza na kupambana na masuala ya UKIMWI ni afua ya ulielimishaji rika ambayo inahusika kukinga na kuelimisha wasichana  rika balehe ili wajiamini  na kupambana na  maisha yao wenyewe pamoja na  kuepuka vishawishi,”Alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera, Bunge  na Uratibu, Kaspar Mmuya  alisema  afua za UKIMWI hazitekelezwi na wizara moja pekee bali zinatekelezwa na  wizara zote za kisekta na wadau  wa ndani na nje ya nchi .

“Malengo ya Serikali katika kupambana na UKIMWI imejielekeza ifikapo mwaka 2030 kusiwe  na maambukizi mapya  ya virusi vya UKIMWI  na pasiwepo  na mtu yeyote mwenye virusi vya UKIMWI ambaye atakufa kwa ugonjwa huo pamoja na kuondoa unyanyapaa ifikapo mwaka 2030,”Alibainisha Mmuya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko  alifafanua tume hiyo inashirikiana  na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo ina mtaala wa uelimishaji rika ambao unafundishwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri 18.

Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Bi. Hanji Godigodi aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za taasisi za Serikali na binafsi zinazopambana kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI huku akiwataka watendaji kusimamia fedha za mradi ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.

Aidha, Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bi. Gladness Champunga aliishukuru Serikali na TACAIDS kwa kuanzisha mradi akisema umemnufaisha kama kijana kujipatia kipato kupitia saluni yake ambapo inamuwezesha kukidhi mahitaji muhimu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi