[caption id="attachment_6292" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akisisitiza jambo kwenye uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Kagera[/caption] [caption id="attachment_6290" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Kagera uliofanyika katika kijiji cha Rwabigaga wilayani Kyerwa. Kulia kabisa ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na kushoto ni Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate.[/caption]
Na Greyson Mwase, Kagera
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema vijiji na vitongoji vyote vya mkoa wa Kagera vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kama sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III)
Dkt. Kalemani aliyasema hayo mapema Julai 11, 2017 kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) utakaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyofanyika katika kijiji cha Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani Kagera pamoja na kumtambulisha mkandarasi atakayefanya ujenzi wa sehemu ya kwanza ya mradi katika mkoa huo.
Alisema utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika mkoa wa Kagera utahusisha vipengele vitatu ambavyo ni pamoja na kusambaza umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme na kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya maeneo na vitongoji havikuungwa.
Waziri Kalemani alisema kipengele cha tatu kinahusisha usambazaji wa umeme utokanao na vyanzo vya nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi hususan visiwani.
Aliendelea kusema kuwa utekelezaji wa mradi huu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya awali itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 141 kwa gharama ya shilingi bilioni 45.43 na kuongeza kuwa utekelezaji wa sehemu ya kwanza ulianza tangu mwezi Februari mwaka huu ambapo inatarajiwa kukamilika mapema Aprili, 2019
Alieleza kuwa kazi hii itafanywa na mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/S Nakuroi Investment Company Limited na kuongeza kuwa sehemu ya pili ya mradi huu wa kusambaza umeme vijijini kwa vijiji 180 vilivyobakia utaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019, hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya mkoa wa Kagera ifikapo mwaka 2021.
Dkt. Kalemani aliwaomba wananchi kutumia fursa ya umeme wa uhakika kwa kuboresha maisha yao kupitia miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma mbalimbali za jamii ili uwekezaji huu wa Serikali ulete manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
“Wananchi sasa ninawaomba mtumie fursa hii ya umeme wa uhakika kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao pamoja na huduma za afya, elimu, maji, kilimo na viwanda vingine, mashine za kusaga, useremala, kuhifadhi vinywaji na vyakula pamoja na kuchomelea vyuma shughuli ambazo zitawapatia kipato na kuboresha maisha yenu,” alisisitiza Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wananchi watakaounganishwa na huduma ya umeme kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili mkandarasi atakapofika katika maeneo yao wawe tayari kulipia na kuunganishiwa na huduma ya umeme.
Aliongeza kuwa, wananchi ambao nyumba zao si kubwa sana wanahimizwa kuomba kufungiwa kifaa maalum kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba.
Waziri Kalemani aliwaomba wananchi kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya umeme bila ya kudai fidia kama mchango wao kwenye mradi huu na kuwezesha fedha iliyotengwa kuunganisha wateja wengi zaidi.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani aliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika mkoa wa Kagera kusogeza huduma karibu na wananchi wa wilaya ya Kyerwa ili kuepuka gharama ya kufuata huduma mbali.
Wakati huo huo akielezea kwa kifupi Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo- Hanga, alisema mradi unalenga kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote Tanzania Bara ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania Bara ina vijiji 12,268 ambapo vijiji vilivyofikiwa na umeme hadi Juni, 2016 vilikuwa ni 4,395 sawa na asilimia 36.
Mhandisi Nyamo-Hanga aliongeza kuwa kati ya vijiji 7,873 ambavyo havijapata umeme, vijiji 7,697 vimepangwa kupatiwa umeme wa gridi na vijiji 176 pamoja na visiwa vitapatiwa umeme wa nje ya gridi kwa kuwa ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa na kusisitiza kuwa mradi huu umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2020/21.