Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

KAGAME ATUA DAR , TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA BIASHARA NA USHIRIKIANO
May 03, 2026
KAGAME ATUA DAR , TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA BIASHARA NA USHIRIKIANO
Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, akiwasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Na Baraka Messa – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa haya mawili jirani.

Rais Kagame ametua leo mei, 3,2026 akiwa jiijini Dar es Salaam,  anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu, yakilenga kukuza ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na maendeleo ya kijamii.

Ziara hiyo imekuja katika kipindi ambacho mahusiano kati ya Rwanda na Tanzania yameendelea kuimarika kwa kasi, yakichagizwa na vikao vya Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC), vinavyolenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.

Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa washirika wakuu watatu wa biashara wa Rwanda duniani, huku kiwango cha biashara kati ya nchi hizo kikiongezeka mwaka hadi mwaka, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi kwa pande zote mbili.

Kwa upande wa uwekezaji, kuanzia mwaka 1990 hadi Machi 2026, Tanzania imesajili jumla ya miradi 42 kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.53, iliyosaidia kuunda ajira 2,225 katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, usafirishaji, huduma za kifedha, maliasili na utalii.

Wakati huo huo, wawekezaji wa Tanzania wameendelea kupanua shughuli zao nchini Rwanda kupitia kampuni mbalimbali, zikiwemo Bakhresa Group, Magodoro Dodoma, Discount Center, Jambo Plastic, Sagar Enterprises, Buffalo Travelling Tours, Maxcom Africa, Gasabo Grain Milling Company, LCM Delta Company na Metrex Integrated Consultancy.

Ziara ya Rais Kagame inatazamwa kama chachu ya kuimarisha zaidi diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizi mbili, huku matarajio yakiwa ni kuibua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira kwa wananchi wa pande zote.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi