[caption id="attachment_36271" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Skauti Mkuu wa Tanzania Ndg. Mwantumu Bakari Mahiza Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 3, 2018[/caption]
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ili kuondoa changamoto zinazoikabili Wizara hiyo na hivyo kuleta ufanisi wa kazi.
Akizungumza mapema leo Ikulu, Jijini Dar es salaam, katika hafla ya kuwaapishwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe na Skauti Mkuu wa Tanzania, Mwantumu Mahiza, Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Augustine Mahiga kufanya mabadiliko kwa viongozi mbalimbali ili kuondoa mazoea ya utendaji usioridhisha ili kuleta ufanisi wa kazi wizarani.
“Sasa ni lazima mfanye mabadiliko bila huruma katika Wizara hii, kwa vile kuna nafasi katika wizara nyingine na kuna baadhi ya viongozi wamekaa wizara hii muda mrefu na wamekuwa wakifanya mambo kwa mazoea yaani businness as usual” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amemsisitizia Balozi Mahiga kufanya mabadiliko hayo makubwa kwa viongozi kiutendaji katika Wizara hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi na kuliletea tija Taifa.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli amempongeza Waziri Dkt. Mahiga kwa kumuwakilisha vyema katika kazi mbalimbali zinazofanyika nje ya nchi. “Unaposafiri unaenda na msaidizi, kuliko angeenda Rais na misafara ya watu wengi, tunaokoa fedha nyingi za wananchi” amefafanua Rais Magufuli
Pia, Katibu Mkuu aliyeapishwa kuitumikia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, ameahidi kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu za kazi pamoja na kufuata maadili ya kiapo.
“Mheshimiwa Rais nakutoa hofu naenda kufanya kazi, naenda kufanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Dkt. Mnyepe
Katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania, Dkt. Magufuli amemuapisha Skauti Mkuu wa Tanzania, Mwantumu Mahiza, na kukitaka Chama cha Skauti kuendelea kufanyakazi nzuri ya kulea vijana katika maadili ya upendo na uzalendo wa kweli.
“ Nimeona yanapotokea majanga mbalimbali mfano tatizo la Ukara, Skauti mnakuwa mbele katika kutoa misaada pale inapohitajika, mimi pamoja na watanzania tunashukuru kwa kazi mnazofanya, endeleeni na tambueni hata mimi niko pamoja nanyi” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Mkuu wa Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza alisema kuwa atajitahidi kuhakikisha kuwa Skauti inawajenga vijana wa Tanzania katika maadili mema hata kuwa mfano wa kuigwa Afrika na duniani.
Naye, Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ally Hassan Mwinyi, amesifia utendaji kazi wa Rais Magufuli kwa kuwa ni wa maslahi ya Taifa na kuahidi kuwa Skauti itaendelea kufanyakazi vizuri ya kuwalea vijana katika maadili, ukakamavu na uzalendo.
Naye Rais wa Skauti Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako (pia Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia) amesema Chama cha Skauti nchini Tanzania kilianzishwa mwaka 1907 kikiwa na lengo la kulea vijana katika misingi ya uzalendo, ukakamavu na kuwajengea uwezo yanapotokea matatizo au majanga mbalimbali.