Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI Yatoa Elimu ya Chanjo kwa Wafanyakazi wa TADB
Sep 24, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Serikali imeandaa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 kwa kuwafuata wananchi wanaohitaji huduma ya chanjo mahali walipo ili kuongeza kasi na kuwapa wananchi nafasi ya kuchanja.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt.  Rashid Mfaume wakati wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipoalikwa na uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo pamoja na kutoa chanjo ya UVIKO - 19 kwa wafanyakazi wa benki hiyo jana Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mfaume alisema kitendo kilichofanywa na JKCI kwa kushirikiana na TADB ni maelekezo ya Serikali kwamba lazima sasa wataalam wa afya watoke na kuwafuata wananchi wenye uhitaji wa chanjo ya UVIKO – 19 pale walipo.

“Tunawapongeza sana uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa kuratibu utapikanaji wa chanjo kwa wafanyakazi, sio benki zote ambazo zinaweza kuratibu upatikanaji wa chanjo eneo la kazi, hii inaonesha utofauti wa benki hii na benki nyingine”,

“Wafanyakazi hawawezi wakafanya kazi wasipokuwa na afya njema, maamuzi mliyoyafanya ya kupata chanjo kwa namna moja ama nyingine mtakuwa mnatekeleza sera zenu”, alisema Dkt. Mfaume.

Akitoa elimu ya umuhimu wa chanjo ya UVIKO – 19 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema mtu anapopata chanjo anakua kwenye nafasi ndogo ya kupata changamoto kubwa za kiafya pale atakapopata ugonjwa wa UVIKO – 19.

“Watu wengi waliopata ugonjwa wa UVIKO – 19 asilimia 85 walipata maradhi madogo madogo kama vile kuumwa kichwa, mafua na homa za hapa na pale, asilimia 10 walifikia hatua za kupata huduma za hospitali kama vile kulazwa na kadhalika, lakini asilimia 5 walifikia hatua za kutumia msaada wa mashine kupumua”,

“Kama leo wote tutachanja ni matumaini yangu hata ikitokea tukapata ugonjwa huu tutaishia kwenye ile asilimia 85 ya kusumbuliwa na maradhi madogo madogo”, alisema Dkt. Waane

Aidha Dkt. Waana amewataka wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 kwa kuendelea kunawa mikono yao kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano pamoja na kuvaa barakoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege alisema  menejimenti ya Benki yake imeona ni vyema kuwapa nafasi wafanyakazi wa benki hiyo ili waweze kupata elimu juu ya ugonjwa wa UVIKO – 19 pamoja na chanjo, kwani kupitia elimu sahihi waliyoipata wengi wao watabadili mawazo potofu waliyokuwa nayo.

“Sisi kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania tumeona kwasababu tuna wadau mbalimbali na tunajihusisha na wakulima wa nchi nzima tusipokuwa mfano kwa wadau wetu uchumi wa nchi yetu unaweza ukatetereka maana watu ambao ni wazalishaji katika mashamba kwa ajili ya kuinua uchumi wetu utuchukulia sisi kama mfano katika maisha yao”,

“Ninaamini baada ya kupata elimu hii ya kisayansi kutoka kwa daktari bingwa wa JKCI Tatizo Waane juu ya chanjo ya UVIKO – 19 hata wale tuliokuwa na mashaka leo tutachukua hatua ya kuchanja, mimi leo nitakuwa mfano hapa kwa kuchanja”, alisema Nyabundege.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi